Habari za Kitaifa

Magavana wakaa ngumu, waendelea kukaidi maagizo ya Serikali Kuu

Na MERCY SIMIYU September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Magavana wameongeza ukaidi dhidi ya maagizo ya Serikali Kuu ambayo wanasema yanadhoofisha mamlaka yao, hatua inayoweka msingi wa mvutano na utawala wa Rais William Ruto.

Ajira ya kudumu kwa wahudumu wa afya, matumizi ya lazima ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma, mfumo mmoja wa ukusanyaji mapato kwa kaunti zote, nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa kaunti, na ucheleweshaji wa mgao wa fedha, ni miongoni mwa malalamishi mapya ya magavana.

Jana, Baraza la Magavana (CoG) lilifanya mashauriano na maafisa wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Waziri Aden Duale, lakini hakukuwa na makubaliano kuhusu kuajiriwa mara moja kwa wahudumu 7,414 wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) na kaunti.

Magavana walisisitiza kuwa hawawezi kuwaajiri wahudumu hao hadi Wizara ya Afya ilipie mafao ya mkataba ya Sh9.4 bilioni na kuhamisha Sh7.7 bilioni kwa kaunti kwa ajili ya mishahara yao chini ya masharti ya ajira ya kudumu na ya pensheni.

Mkutano huo uliamua kuwa wahudumu hao wataendelea kufanya kazi chini ya mikataba yao ya sasa hadi mwaka ujao, mikataba hiyo itakapokamilika.

“Baraza la Magavana na Wizara ya Afya walikubaliana kuwa, kwa manufaa ya wahudumu wa UHC na umma kwa ujumla, mpito huo utafanyika tu ikiwa rasilmali zinazohitajika – Sh7.7 bilioni  zitapelekwa kwa serikali za kaunti kupitia Sheria ya Mgao wa Mapato na mgao wa haki wa mapato utaongezwa,” alisema Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi.

Hadi wakati huo, magavana wamesema kuwa wahudumu hao watalipwa kulingana na viwango vya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), kwa kutumia fedha kutoka Wizara ya Afya.

CoG ilitangaza kuundwa kwa kamati ya pamoja ikijumuisha wenyeviti wa kamati za Afya, Sheria, Fedha na Wafanyakazi kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya ili kukubaliana jinsi ya kuwalipa wahudumu hao kulingana na viwango vya SRC hadi mikataba yao itakapokamilika.

Waziri wa Afya Bw Aden Duale alihakikisha kuwa Sheria ijayo ya Mgao wa Mapato, inayotarajiwa katika mwaka wa fedha ujao, itajumuisha Sh7.7 bilioni zinazohitajika.

“Fedha hizo zitajumuishwa kwenye Mswada wa Mgao wa Mapato na ndipo suala la wahudumu wa UHC litakamilika,” alisema Bw Duale, ambaye agizo lake la hivi majuzi la kaunti kuwaajiri wafanyakazi hao kufikia Septemba 1 ndilo lililosababisha mzozo huo.

Viongozi wa kaunti pia wametaka kufutiliwa mbali kwa mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa serikali (e-GP) unaoungwa mkono na Wizara ya Fedha, ambao Rais Ruto amesisitiza hautasitishwa, na pia wamekataa presha kutoka kwa serikali  kutumia mfumo mmoja wa ukusanyaji mapato unaofanana na e-Citizen kwa kaunti zote 47.

Magavana wanataka nyongeza ya Sh4.8 bilioni  ili kutekeleza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa kaunti. Wanasema kuwa serikali kuu tayari ilitekeleza mapitio ya mishahara kwa wafanyakazi wake wote katika mwaka wa fedha wa 2024/25.

Baraza la Magavana, chini ya uenyekiti wa Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi, linataka Wizara ya Fedha kusitisha utekelezaji wa lazima wa mfumo wa e-GP.

“naitaka Wizara ya Fedha kuondoa mara moja barua iliyotuma kuzitaka kaunti kuanza kutumia mfumo wa e-GP hadi mashauriano, upangaji wa kisheria na mafunzo ya uwezo yafanyike ipasavyo,” liliongeza Baraza hilo.

Masuala haya tata yanaongezea kwenye orodha ndefu ya malalamishi ya muda mrefu kama vile mgao wa mapato ya kitaifa kati ya serikali kuu na kaunti, na ucheleweshaji mkubwa wa mgao wa fedha.

Mwaka huu, magavana walitaka Sh536.9 bilioni  lakini Hazina ya Kitaifa ilipendekeza Sh405 bilioni  kama mgao wa haki kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.

Ili kufungua mkwamo kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu Mswada wa Mgao wa Mapato 2025, mgao wa haki kwa kaunti uliwekwa kuwa Sh415 bilioni.

Jana, magavana kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, walikubaliana kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia jinsi fedha kutoka kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) zinavyotolewa kwa vituo vya afya vya kaunti. Walibainisha kuwa kaunti bado hazijalipwa madai ya fedha.

Baraza pia lilikosoa Tume ya Huduma za Umma (PSC) kwa kutunga miongozo ya ukuaji wa kazi kwa wahudumu wa afya bila kushauriana na kaunti.

“Tunaomba PSC kuondoa miongozo hiyo na kuepuka kuidhinisha miongozo inayotegemea nyadhifa maalum kwa kuwa ina athari kubwa kifedha kwa kaunti bila kuzingatia gharama ya utekelezaji katika mgao wa haki wa mapato,” walisema magavana.