Magavana wanavyozama kwenye madeni wakisaka pesa za kulipa mishahara
MAGAVANA kadhaa wamelazimika kuchukua mikopo yenye riba ya juu kutoka kwa benki kufadhili matumizi ya kawaida, ambayo ni pamoja na ulipaji wa mishahara na huduma muhimu.
Hatua hiyo inanuia kuhakikisha kuwa shughuli muhimu za kaunti hazilemazwi kwani Hazina ya Kitaifa imekosa kutoa pesa zinazotarajiwa na kaunti kila mwezi.
Ripoti ya hivi punde ya utekelezaji wa bajeti ya miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o, imebaini kuwa baadhi ya kaunti zililazimika kuchukua mikopo kuendeleza shughuli zao.
Kulingana na ripoti hiyo, katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka inayoangaziwa, kaunti nane zilikopa zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa benki za biashara ili kuendeleza shughuli na kulipa mishahara ya wafanyikazi.
Kaunti zilizoathirika ni pamoja na Kisumu, Kakamega, Kisii, Migori, Laikipia, Homa bay, Bungoma na Nyandarua. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kwamba mikopo hii, pamoja na kucheleweshwa kwa malipo, huweka serikali za kaunti hatarini kulipa faini kubwa na riba ya juu na kutishia zaidi miradi ya maendeleo inayoendelea.
“Mikataba hiyo inatishia kulemaza miradi ya maendeleo katika kaunti kwani magavana watalazimika kurekebisha bajeti zao ili kulipa faini na riba inayotokana na mikopo hiyo,” akasema Bw David Ngugi, mtaalamu wa masuala ya utawala.
“Kaunti tayari zinatatizika kulipa madeni. Ziko katika hatari ya malimbikizi ya madeni zaidi kutokana na adhabu, kwani nyingi hazipeleki michango ya wafanyikazi kwa mashirika kama NSSF na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA), ambayo inaweza kuzifanya kulipa faini zaidi.”
Huku zikikabiliwa na ucheleweshaji wa pesa kutoka Hazina ya Kitaifa, baadhi ya kaunti zimeweka Mkataba ya Makubaliano (MOUs) na benki ili kudhibiti malipo ya mishahara wakati wa uhaba wa pesa taslimu, na kukubali kurejesha mikopo hiyo mara pesa zitakapotolewa.
Kwa mfano, Kaunti ya Homa Bay ilikopa Sh473.69 milioni kutoka Benki ya KCB na Benki ya Equity kusaidia shughuli wakati wa uhaba wa pesa.