Magavana wanawake walaani biashara haramu ya ngono
KUNDI la Magavana wa Kike nchini, maarufu kama G7, limekemea vikali biashara haramu ya ngono inayohusisha watoto, hasa wasichana, katika eneo la Mai Mahiu.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, kundi hilo likiongozwa na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, lilieleza kuwa unyanyasaji wa kingono na ulanguzi wa watoto ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ni shambulizi la moja kwa moja kwa utu, usalama, na mustakabali wa watoto hasa wa kike.
Taarifa hiyo inafuatia ripoti ya kituo kimoja cha kimataifa cha habari kilichofichua mtandao wa ukahaba Mai Mahiu, ambapo wanawake wakubwa wamekuwa wakiwauza wasichana wadogo kwa wanaume kushiriki ngono.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa wengi wa wasichana hao walitoroka nyumbani kutokana na mazingira ya dhiki kama vile kuwa yatima au kuishi katika umaskini, kabla ya kutumbukia kwenye unyanyasaji wa kingono.
Baadhi ya watoto hao walikiri kulazimishwa kushiriki ngono bila kinga, hali inayowaweka hatarini kuambukizwa maradhi kama Ukimwi.Magavana hao walitoa wito kwa serikali kuanzisha uchunguzi wa haraka na kuwachukulia hatua kali wahusika wote iwe ni wauzaji, wasaidizi wao, au wateja.
Walisisitiza pia kuwa maafisa wa usalama waliotelekeza wajibu wao au kushirikiana na wahalifu hao wanafaa kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Janga hili linaonyesha kushindwa kwa jamii na linahitaji hatua ya haraka na ya pamoja.Hatupaswi kufumba macho wakati watoto wananyang’anywa utoto wao, kudhulumiwa na kutumika kwa kisingizio cha umaskini na ukosefu wa uwajibikaji,” taarifa yao ilisema.
Viongozi hao wa kike pia walieleza kuwa watoto wanaohusika wanahitaji msaada wa dharura wa kisaikolojia, matibabu, na elimu ili kuanza maisha upya. Walitaka kuanzishwa kwa mpango wa pamoja wa serikali wa kuwaokoa, kuwahudumia, na kuwaunganisha tena na jamii.
“Kinachotendeka kwa watoto wetu Mai Mahiu ni cha kusikitisha na hakiwezi kuvumiliwa. Kama G7, tunasimama pamoja tukitaka hatua za dharura zichukuliwe kuwaokoa watoto hawa, kuwalinda, na kurejesha maisha yao. Kila mhusika lazima awajibishwe,” alisema Gavana Waiguru kwenye mitandao yake ya kijamii.
Viongozi hao walikiri dhamira yao ya kulinda haki za watoto katika kila kaunti na wakaahidi kushirikiana na mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini, viongozi wa jamii, na washirika wa kimataifa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto hasa katika maeneo yaliyoathirika na umaskini na uhamaji.