• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Waiguru achaguliwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana

Waiguru achaguliwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG).

Bi Waiguru wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ndani ya muungano wa Kenya Kwanza amechaguliwa Jumamosi katika kongamano la magavana na manaibu wao lililofanyika mjini Mombasa kuwapa mafunzo ya uongozi hasa wale wapya.

Amekuwa gavana wa kwanza wa kike kuongoza baraza hilo, tangu kuzinduliwa kwa serikali za ugatuzi mwaka 2013.

Gavana huyo amemenyana na kumbwaga mwenzake wa Kajiado, Joseph Ole Lenku wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Waiguru anarithi nafasi hiyo kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora ambaye alimaliza mihula yake miwili kama mkubwa wa kaunti yake kwa mujibu wa Katiba.

“Nathibitisha kwamba zoezi la kuchagua uongozi wa CoG lilikuwa shwari. Magavana waliafikiana kupitia idadi kuhusu waliochaguliwa,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, Mary Mwiti.

Gavana wa Wajir, Ahmed Abdullahi alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti naye Gavana wa Nandi Stephen Sang ndiye atakuwa kiranja.

Bi Waiguru anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho kama Gavana wa Kirinyaga.

Alihifadhi kiti chake kupitia chama cha UDA, kinachoongozwa na Rais William Ruto.

Dkt Ruto pia ndiye kinara mkuu wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

CBC: Mbunge adai walimu wamechosha wazazi kwa kutaka kuku...

Muungano wa Kenya Kwanza waibuka na wawaniaji wake wa...

T L