Magenge ya Haiti yavamia miji licha ya juhudi za polisi wa Kenya kukomboa maeneo
SIKU chache baada ya wakazi wa Port-Sonde nchini Haiti kurejea makwao kufuatia shambulizi lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 70, magenge ya majambazi sasa yanalenga miji mbalimbali katika taifa hilo.
Wiki iliyopita, wanachama wa genge hilo lenye ngome yake Viv Ansanm, waliharibu kituo kipya cha polisi katika eneo la Cabaret ambacho kimekuwa chini ya uongozi wa maafisa wa polisi Haiti (HNP).
Washambulizi walikuwa wamevalia mavazi yaliyokuwa na nembo ya Unite Village de Dieu (UVD).
Magenge hayo yalivamia kituo hicho saa 24 baada ya oparesheni ya kimataifa inayoongozwa na Kenya (MSS) pamoja na HNP kuteka mji wa Cabaret.
“Magenge hayo bado yanadhibiti miji kadhaa mjini Haiti, hata hivyo, ninafahamu wakazi wa Port-Sonde, walioshambuliwa majuzi na zaidi ya 70 kufa, sasa wanarejea makwao,” alisema Bw Wethzer Piercin.
Miji mingine ambayo ingali na misukosuko kutokana na mashambulizi yanayoendelea ni pamoja na Solino na Arcahaie ambapo watu kadhaa wametoroka makwao.
Hata hivyo, wiki hii, Kamanda wa Misheni ya MSS Geoffrey Otunge, alisema wakazi wa Port-Sonde hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa sababu wameimarisha usalama eneo hilo.
“Watu wanaoishi Port-Sonde wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kawaida kwa sababu tumeweza kuimarisha usalama eneo lote.
Alisema haya huku wakazi wakielezea wasiwasi kuwa wanatishiwa.
Oktoba 4, 2024, watu wasiopungua 70 waliuawa wakati wanaume waliojihami kutoka genge la Gran Grif waliposhambulia eneo la Port-Sonde eneo la katikati Haiti.
Wakati wa shambulizi hilo, wanachama wawili wa genge hilo walijeruhiwa vibaya kufuatia hatua iliyochukuliwa na maafisa wa HNP.
Jumla ya makazi 45 waliangamziwa na magari zaidi ya 30 kuteketezwa na genge hilo huku wakazi wakikimbilia usalama wao.
Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille, alilaani shambulizi hilo akisema halikufaa kwa sababu lililenga wanawake na watoto wasio na hatia.
“Kwa wanaopanda ugaidi, nasema hivi, hamtalegeza nia yetu. Hamtateka watu hawa ambao wamekuwa wakipigania hadhi na uhuru wao, Hatutawahi kufa moyo kuhusu haki yetu ya kuishi kwa amani, usalama na haki,” alisema Bw Conille.
Genge la Gran Grif linaongozwa na Luckson Elan ambaye baada ya shambulizi hilo alishutumu polisi kwa kuua wanachama wa genge hilo.