Mahakama yasikia kilio cha Ruto
NA SAM KIPLAGAT
MAHAKAMA ya Rufaa imeruhusu serikali kuendelea kukata ushuru wa nyumba za gharama nafuu hadi pale itatoa uamuzi wake mnamo Januari 26, 2024.
Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alifika kortini na kunyenyekea mbele ya mahakama hiyo kwa niaba ya serikali ambapo aliiambia kwamba ushuru huo ulikuwa tayari umesaidia kubuni nafasi za ajira 120,000.
Soma Pia: Ruto ainyenyekea mahakama aruhusiwe kukata ushuru wa nyumba
Majaji walioruhusu serikali kuendelea kukata ushuru huo ni Lydia Achode, John Mativo, na Mwaniki Gachoka.
“Hali iendelee jinsi ilivyo kwa sasa hadi uamuzi kuhusu kesi hii utakapotolewa,” wamesema majaji hao.
Mwanaharakati Okiya Omtatah aliwasilisha kesi ya kupinga ushuru wa nyumba ambao wafanyakazi hutozwa asilimia 1.5 ya mishahara yao, akisema kwamba ni ushuru wa kiubaguzi.
Mnamo Novemba 28, 2023, Mahakama Kuu ilibatilisha ushuru huo, lakini ikasema inaipa serikali hadi Januari 10, 2024, kukata rufaa.