Makanda kusimamia jopo la kuteua makamishna wa IEBC
JOPO la uteuzi wa makamishna tisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo Ijumaa, Januari 31 lilichagua Nelson Makanda na Lindah Kiome kama Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, mtawalia, huku likianza kazi.
Jopo hilo lilijipa muda usiozidi siku 85 kukamilisha mchakato ambao ni pamoja na kupokea maombi, kuorodhesha majina na kufanya mahojiano kabla ya kuwasilisha majina ya watu waliohitimu kwa Rais kuteuliwa makamishna wa IEBC.
“Kwa muda wa siku 85 au chini ya hapo, sisi, kama jopo la uteuzi, tumejitolea kuhakikisha kwamba tunatimiza wajibu wetu wa kuwapa Wakenya mwenyekiti ajaye na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,” alisema Dkt Makanda kwenye taarifa.
“Jopo hilo kesho Jumamosi, Februari 1, 2025, litaalika maombi kutoka kwa Wakenya waliohitimu kwa nafasi za Mwenyekiti na makamishna wa IEBC. Ninawahakikishia Wakenya kuwa Jopo la Uteuzi limejitolea kuendesha zoezi kwa njia isiyo na upendeleo, ya haki na ya uwazi,” akasema.
Jopo la watu tisa walioapishwa ni pamoja na Dkt Makanda na Fatuma Saman, waliopendekezwa na Baraza la Dini mbalimbali la Kenya; Bi Kiome na Prof Adams Oloo kuwakilisha Tume ya Huduma za Bunge; Bw James Misati, Bw Nicodemus Bore na Dkt Koki Muli wa Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Kisiasa (PPLC).
Bw Andrew Kipkoech Tanui anahudumu katika jopo kuwakilisha Taasisi ya Uhasibu wa Umma Kenya, huku Bi Carolene Kituku akiwakilisha Chama cha Wanasheria nchini Kenya.
Jopo hilo lilitoa ahadi hiyo huku kundi la mashirika ya kijamii likiwataka wanachama kudumisha uwazi na uhuru katika kuunda upya IEBC.
Shughuli ya kuajiri Makamishna wapya wa IEBC imekuwa mchakato mrefu na wenye utata tangu kukamilika kwa muda wa walioongozwa na Wafula Chebukati.
Mnamo Januari 2023, muda wa kuhudumu kwa Chebukati kama Mwenyekiti na Makamishna Abdi Guliye na Boya Molu, uliisha. Wengine watatu—Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, na Francis Wanderi—walijiuzulu, huku Bi Irene Masit akifukuzwa kazi baada ya mchakato wa mahakama na kuiacha tume ya uchaguzi bila makamishna kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA