Habari za Kitaifa

Makanisa yanavyofyonza pesa za wazazi kwa kutoa huduma ghali za tohara

November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKANISA na mashirika ya kidini kwa mara nyingine yameanza kufyonza fedha kutoka kwa wazazi kwa kutoa huduma za upashaji tohara miongoni mwa wavulana.

Baadhi ya makanisa hayo yameanza kuvumisha huduma katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ambapo wanatoza hadi Sh50,000 kwa kila mvulana.

“Tumepandisha ada ya huduma zetu hadi Sh50,000 kutokana na ongezeko la ushuru na kupanda kwa gharama ya maisha. Aidha, marafiki na jamaa wanaoandamana na familia siku ya wavulana kurudi nyumbani baada ya kupona watalipa Sh400 kwa kadi za chakula,” kulingana na usimamizi wa Eldoret Adventist Resort.

Chini ya mpango huo, unaotofautiana na tohara za kitamaduni zinazofanyika katika msimu kama huu wa likizo ndefu, wazazi huwapeleka watoto wao katika makanisa na mashirika husika kupashwa tohara na kupewa uhamasisho kuhusu majukumu ya utu uzima.

Lakini ada ambazo mashirika haya yanatoza mwaka huu ni ya juu zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Makanisa hayo yanawavutia wazazi na walezi kwa kuwaambia kuwa huduma zao zinajumuisha ushauri nasaha, ushauri wa kitaaluma na ushauri kuhusu masuala ya kitamaduni.

Aidha, makanisa yanadai ada zao zinajumuisha gharama ya madaktari wenye ujuzi, dawa bora, vyakula vyenye madini na mavazi bora ya kuvaliwa wavulana wanapohitimu baada ya mpango huo wa wiki tatu.

“Kutokana na changamoto zinazokabili kizazi cha sasa, watoto wetu wanahitaji kuhamasishwa kuhusu haja ya kufanya maamuzi bora kwa mustakabali wao. Tunawaondolea wazazi mzigo huo kwa kutoa huduma kama hizo,” inasema Eldoret Adventist Resort.

Kituo cha Kapkoros Mentorship Centre, kilichoko Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu, kinatoza ada ya Sh40,000 kwa kila mvulana kwa mpango huo unaodumu kwa kupindi kwa mwezi mmoja.

“Tunalenga kuwafunza wavulana ili wawe wanaume wa Kikalenjin wanaowajibika huku wakilenga kusajiliwa katika vyuo vya kiufundi mwaka ujao,” ikasema notisi iliyowekwa na usimamizi wa kituo hicho.

“Tofauti na vituo vingine, tunadumisha utamaduni wetu tunapowaelekeza vijana wetu ili waingie katika utu uzima na wawe wanajamii wanaowajibika,” akaeleza mmoja wa wazee aliyeomba tulibane jina lake.

Inasema kuwa huduma za upashaji tohara na mafunzo kwa wavulana zinaweza kugharimu hadi Sh250,000 kwa kila mvulana kwa familia za matajiri, haswa katika maeneo ya mijini.

“Tunachoshuhudia hapa ni kuibuka kwa matabaka mawili ya wanaopashwa tohara. Wale ambao wanaweza kumudu ada za juu na wale ambao wameamua kudumisha tohara ya kitamaduni ambayo si ghali,” akasema James Maina, mzee mmoja kutoka eneo la Saos, Kaunti ya Nandi.

Alisema kuwa madhara yanayotokana na upashaji tohara visivyo na ghariba wa kitamaduni ndio huchangia wazazi kukumbatia huduma za kisasa za upashaji tohara.

Mwaka jana wavulana 15 kutoka kaunti ya Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet wanadaiwa kufariki dunia kutokana hitalafu zilizotokea wakipashwa tohara kitamaduni.