Malala atupwa katika kapu la ‘utajua hujui,’ avuliwa rasmi wadhifa wa Katibu Mkuu wa UDA
CHAMA cha United Democratic Alliance UDA kimemfuta kazi rasmi Katibu wake mkuu Cleophas Malala baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho uliofanyika Ijumaa.
Kutokana na kufutwa kazi kwa Malala, Hassan Omar Hassan ameteuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu.
“Uteuzi wa Mheshimiwa Cleophas Malala kuwa Katibu Mkuu wa muda umebatilishwa. Mabadiliko haya yanaanza kutekelezwa mara moja,” ilisema sehemu ya taarifa ya UDA.
Haya yamejiri siku mbili baada ya sarakasi kushuhudiwa katika makao makuu ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Jumanne, Julai 30, 2024 baada ya baadhi ya wanachama kutaka kumwondoa Malala afisini.
Wakiongozwa na wakili Joe Khalende, kundi hilo lililojiita “Waanzilishi wa UDA” lilimsuta Malala likidai anadumaza maendeleo ya chama hicho na Serikali Jumuishi iliyoundwa na kiongozi wa chama, Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Khalende na wenzake pia walimshutumu Bw Malala kwa kushirikiana na viongozi wa Vuguvugu la TAWE linaloongozwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, hivyo kukiuka Katiba na mwongozo wa UDA.
Akiongea na wanahabari, wakili huyo alijitangaza kuwa kaimu mpya wa Katibu Mkuu wa UDA na kwamba Malala amepigwa marufuku kuendesha majukumu yote ya afisi hiyo.
“Malala ametelekeza wajibu na majukumu yake kama Katibu Mkuu wa chama chetu cha UDA. Miongoni mwa majukumu hayo ni kuwa msemaji wa chama na kuitisha mikutano yote. Yeye ameungana na wapinzani wetu. Anaunga mkono vuguvugu la TAWE na ajenda ambazo zinakinzana kabisa na za chama chetu ambacho ndicho chama tawala nchini,” Bw Khalende alisema.