Habari za Kitaifa

Maseneta wakemea kamati kwa kuchelewesha kuhamisha mali ya kaunti

Na COLLINS OMULO April 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASENETA wameikosoa Kamati ya Kiufundi ya Mahusiano ya Kiserikali (IGRTC) wakisema “haina makali” huku kaunti zikiendelea kusubiri mali zinazopaswa kupata kutoka serikali kuu miaka 12 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi.

Maseneta hao wamesema sasa watachukua jukumu la kuzungumza moja kwa moja na serikali kuu ili kuharakisha uhamishaji wa mali ya thamani ya mabilioni kutoka kwa serikali kuu hadi serikali za kaunti.

Hatua hii inafuatia malalamishi kutoka kwa magavana kwamba bado hawajapokea mali zilizopewa kaunti kutoka kwa serikali kuu licha ya IGRTC kuwa na jukumu la kushughulikia uhamishaji wa mali inayohamishika na isiyohamishika.

Tangu kupitishwa kwa Katiba ya 2010, kukamilika na kuhamishwa kwa mali iliyomilikiwa na yaliyokuwa mabaraza ya miji na inayohusiana na majukumu yaliyopewa serikali za kaunti kumekuwa kukicheleweshwa kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Umma na Fedha Maalum katika Seneti, Godfrey Osotsi, alisema kuchelewa kuhamisha mali isiyohamishika kumekuwa tatizo kubwa, huku Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, akiashiria kuwa kaunti hazina rejista ya kudumisha mali isiyohamishika.

Seneta wa Vihiga alisema kuwa taasisi hiyo imefanya kidogo tu kuhusu uhamishaji wa mali hizo, ikihamisha tu mali kama pikipiki huku mali nyingine ya thamani kubwa ikikosa kuhamishwa.

Aliwataka magavana kusaka suluhisho kupitia Seneti, Baraza la Kiserikali ya Bajeti na Uchumi ili kuhakikisha kuwa mali yote ya majukumu yaliyopewa serikali za kaunti ambayo bado inashikiliwa na serikali kuu inahamishwa.

“Tuna wasiwasi kuhusu IGRTC katika suala la kuhamisha mali. IGRTC inathibitisha kuwa haina meno katika suala hili. Kama Baraza la Magavana, mnapaswa kutafuta njia nyingine ya kushughulikia jambo hili,” alisema Bw Otsotsi ambaye ni Naibu Kiongozi wa ODM.

“Kamati hii itashughulikia suala hili kwa sababu IGRTC imeshindwa kutimiza wajibu wake kuhusu uhamishaji wa mali,” aliongeza.

Seneta wa Elgeyo Marakwet, William Kisang, alisema kuwa Seneti inapaswa kuchukua msimamo rasmi kwa njia ya azimio ambalo litakuwa sheria.

“Tunapaswa kuwasilisha hoja ya kupatia Hazina ya Taifa muda maalum kuhamisha mali inayoshikilia kwa sababu hili litaendelea kuwa tatizo katika ukaguzi milele,” alisema Bw Kisang.

“Tunaweza kuwapa miezi sita kutekeleza azimio letu na kuhakikisha kuwa mali yote inayopaswa kuhamishwa kwa kaunti inahamishwa,” aliongeza.