Habari za Kitaifa

Mashirika ya kijamii yamtaka rais kukabiliana na mauaji ya wasichana na wanawake

Na PAULINE ONGAJI October 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA ya kijamii yamemtaka Rais William Ruto amteue waziri wa masuala ya jinsia ili kukabiliana na visa vya mauaji ya wasichana na wanawake.

Katika kikao na wanahabari hapo Jumanne, wawawikilishi kutoka mashirika kadhaa ikiwa ni pamoja na—Muungano wa mawakili wanawake FIDA-Kenya, Siasa Place, Centre for Community Development and Human Rights, muungano wa wanawafunzi wa vyuo vikuu nchini (KUSO), Child Space Nairobi, Kibera Justice Centre, Inspire Teenagers, na Superb Nairobi—walisisitiza kwamba uteuzi huu ni muhimu katika kuangazia visa vya mauaji ya wanawake na wasichana ambavyo vimekithiri.

Mwenyekiti wa FIDA-Kenya Christine Kungu (kushoto) na makamu wa rais wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Mwaura Kabata wakihutubu Jumanne ambapo walitaka hatua zichukuliwe kukabili mauaji ya wasichana na wanawake. Picha|Evans Habil

Makundi hata yalitoa orodha ya madai kadhaa ikiwa ni pamoja na kwa Rais Ruto kuhutubia taifa moja kwa moja, kukiri kwamba mauaji ya wasichana na wanawake ni janga la kitaifa, na kuhakikisha kwamba serikali imejitolea kulinda haki za wanawake.

Aidha, pia walitoa mwito kwa Idara ya upelelezi wa jinai (DCI) kutoa taarifa kamili kuhusu kesi zinazoendelea kuhusu mauaji ya aina hii, na hasa ile ya Collins Jumaisi, mshukiwa mkuu katika msururu wa visa vya mauaji, ambaye hadi sasa hajulikani aliko baada ya kutoweka kutoka mikononi mwa polisi.

Huku yakiiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya visa hivi hasa tunapokaribia maadhimisho ya siku 16 dhidi ya dhuluma za kijinsia, mashirika hayo yalitaka kuwe na mabadiliko ya kisheria kuainisha mauaji ya aina hii kama hatia kivyake, kuambatana na kanuni ya adhabu.

Akizungumza katika kikao hicho, Bi Christine Kungu, Mwenyekiti wa FIDA-Kenya, alikashifu ongezeko la visa vya mauaji dhidi ya wasichana na wanawake, akisistiza kwamba sharti rais achukue msimamo mkali dhidi ya janga hili.

“Tunachukua msimamo mkali dhidi ya visa hivi nchini kote na vsa hivi vya dhuluma dhidi ya wanawake vinahitaji kukabiliwa vikali na sekta zote husika zikiongozwa na Serikali ya Kenya,” alisema Bi Kungu.

Mwenyekiti wa FIDA-Kenya Christine Kungu (kushoto) na wakili wa shirika hilo Janet Anyango wakisisitiza kuteuliwa waziri wa masuala ya jinsia nchini. Picha|Evans Habil

Aidha akizungumza katika kikao hicho, Bw Mwaura Kabata, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini LSK, alisisitiza kwamba visa hivi vya mauaji vimekuwa janga la dharura ambalo limeathiri usalama na haki ya wasichana na wanawake.

Kulingana na Bi Kung’u, mwaka huu pekee, FIDA-Kenya imenakili takriban visa 30 vya wanawake waliouawa na wapenzi wao, huku idadi kubwa ya visa hivi vikiwa havijapelelezwa vilivyo na Idara ya polisi nchini.

Mashirika haya yaliangazia mauaji ya Bi Yvonne Jirangwa, 23, mtawa wa Kikatoliki aliyepatikana akiwa amefariki katika bomba la kupitisha majitaka.

Mashirika hayo yalionya kwamba ikiwa hatua yoyote haitachukuliwa katika kipindi cha siku 30 zijazo, wataandaa maandaano nchini kote kudai usalama na haki za wanawake.

“Hatuwezi endelea kuruhusu mauaji ya wasichana na wanawake kuwa jambo la kawaida katika jamii yetu,” alisema Kung’u. “Kila msichana na mwanamke yuko huru kuishi maisha salama pasipo kuwepo tishio la dhuluma.”