Maswali 10 yatakayozamisha au kuokoa Koome, majaji
MAHAKAMA Kuu inatarajiwa kushughulikia maswali 10 muhimu yatakayoamua hatima ya majaji wa Mahakama ya Juu akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome katika vita vyao na Tume ya Huduma ya Mahakama.
Miongoni mwa maswali muhimu ni iwapo JSC ina mamlaka ya uangalizi kwa Mahakama ya Juu zaidi.
Swali la pili ni kama yalikuwa makosa kwa JSC kuanzisha kesi ya kuwatimua majaji saba. Mahakama Kuu itaamua kama kulikuwa na ukiukaji wa taratibu na ukosefu wa busara kwaJSC.
Swali la tatu la msingi linahusu uamuzi wa JSC wa kukubali malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya majaji kwa pamoja na wala si kwa kila jaji binafsi.
Swali la nne ni kuhusu madai ya kutofaa kwa uamuzi wa JSC wa kudaiwa kutangaza kwa umma kuwa kulikuwa na malalamishi kuhusiana na kuondolewa afisini kwa majaji wakuu kabla ya kuwafahamisha rasmi majaji husika.
Swali la tano linaibuka katika kesi ya Jaji Isaac Lenaola, likihoji iwapo Jaji Mkuu anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na uamuzi au hukumu iliyotolewa na mahakama lakini ambayo hakuhusika nayo.
Swali la sita ni iwapo JSC inaweza kutumia Kanuni za Huduma za Mahakama kushughulikia malalamishi bila kutangaza sheria hizo kwanza kwenye gazeti la serikali.
Swali la saba linahusu madai ya ukiukaji wa uhuru wa mahakama na JSC, utumiaji wa sheria ya mahakama na iwapo JSC inaweza kushughulikia malalamishi kuhusu kesi ambayo bado haijashughulikiwa katika mahakama nyingine.
Swali la nane linatokana na kesi ya Jaji Mohammed Ibrahim, anayetaka mahakama kubaini iwapo kunaweza kuwa na makosa ya pamoja au ya pamoja ya majaji.
Swali la tisa ni iwapo JSC ilifeli katika jukumu lake la kuwalinda majaji kwa kuruhusu shutuma za ulaji hongo na ufisadi dhidi ya majaji wakuu kuendelea kupeperushwa kwenye mitandao ya kijamii bila walalamishi kumtambulisha mtu yeyote.
Swali la kumi ni ikiwa Jaji Mkuu anaweza kuondolewa ofisini kwa kuzingatia maamuzi ya pamoja ya Mahakama ya Juu.