Maswali DCI ikikaangwa kuhusu miili iliyoopolewa Kware
INAONEKANA mkono wa polisi huwa mrefu sana kwa washukiwa wa mauaji ya raia katika visa vya kijinai visivyohusisha maafisa wa vyombo vya usalama ama visivyoibua hisia kali kote nchini.
Hii ni kauli ambayo inasambaa kama moto jangwani kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na kukamatwa kwa mshukiwa wa mauaji ya Kware, Pipeline, jijini Nairobi.
Maswali mengi yanaulizwa kwa sababu gani kituo cha polisi cha Kware kiko karibu na timbo la Kware lililosheheni miili ya watu waliochinjwa na kutupwa bila kujulikana tangu 2022?
Mshukiwa Collins Khalisia aliishi mtaa wa Soweto, Kayole katika makao ya chumba kimoja mita 500 kutoka timboni
Nao umbali wa kituo cha polisi kutoka timboni ni kilomita moja tu.
Inakuaje polisi wanaishi na muuaji aliyetupa miili ya watu 42 waliochinjwa katika kipindi cha miaka miwili bila kung’amua?
Chupi za wanawake
Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi wa Uhalifu (DCI) Mohamed Amin aliripoti kuwa mshukiwa wa mauaji alikiri kubaka wanawake aliowateka kabla ya kuwaua kikatili.
Na miongoni mwa vitu vilivyopatikana nyumbani mwake ambavyo DCI inatumia kama ithibati ni chupi mbili za wanawake.
Katika mitandao ya kijamii, watumiaji wamepinga hoja hizo kuwa ushahidi wakisema zilikuwa safi sana na zilionekana mpya.
“Chupi yenye sehemu nyeupe upande wa mbele, inaonekana kuwa chupi mpya. Kama aliyevamiwa alikuwa kavaa, ingekuwa na madoa ama na unyevu?” alisema mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii.
Huku maswali mengi yakiulizwa, makachero wanarai raia kuwa watulivu na wakome kukisia chochote hadi uchunguzi kamili ukamilishwe na sheria ichukue mkondo wake.