Maswali kuhusu gharama ya kufuta dili za Adani huku ile Sh104bn ya Afya ikinyamaziwa
RAIS William Ruto alifanya uamuzi wa kijasiri wa kuamuru kufutwa kwa kandarasi mbili za kampuni tata ya Adani Group, huku maswali yakiibuka kuhusu gharama ya kufuta moja ya kandarasi ambayo tayari imetiwa saini, pamoja na hatma ya kandarasi nyingine ya Sh104 bilioni ya mfumo mpya wa Afya, UHC.
Kampuni ya Adani Energy Solutions mnamo Oktoba ilitia saini mkataba wa Sh96 bilioni na Kampuni ya Kusambaza Umeme ya Kenya (KETRACO) kujenga na kuendesha laini nne za usambazaji umeme na vituo viwili vidogo kwa miaka 30.
Kundi la Adani pia lilikuwa katika harakati za kutia saini mkataba mwingine wa Sh238 bilioni na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) kwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Rais mnamo Alhamisi aliagiza mashirika ya ununuzi chini ya wizara ya Uchukuzi na Kawi, mtawalia, kufuta zabuni hizo siku moja baada ya Bw Gautam Adani, Mwenyekiti bilionea wa kampuni hiyo, kushtakiwa Amerika kwa madai ya kutoa hongo ya mabilioni na ulaghai. Waendesha mashtaka wa Amerika walisema Adani na washtakiwa wengine saba, akiwemo mpwa wake Sagar Adani, walikubali kutoa hongo ya Sh34 bilioni kwa maafisa wa serikali ya India.
“Niliwahi kusema huko nyuma, na narudia tena leo, kwamba nikipata ushahidi usio na shaka au taarifa za kuaminika kuhusu hongo, sitasita kuchukua hatua madhubuti,” alisema Rais.
Aliendelea: “Kwa hiyo, sasa naelekeza – katika kuendeleza misingi iliyoainishwa katika Ibara ya 10 ya Katiba kuhusu uwazi na uwajibikaji, na kwa kuzingatia taarifa mpya zilizotolewa na vyombo vyetu vya uchunguzi na mataifa washirika – kwamba mashirika ya ununuzi ndani ya Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Kawi na Petroli yafute mara moja mchakato unaoendelea wa shughuli ya upanuzi kati ya Sekta ya Umma na Sekta ya kibinafsi katika JKIA, pamoja na laini ya usambazaji ya KETRACO iliyokamilika hivi majuzi,” rais alisema..
Hata hivyo kufutwa kwa mikataba hiyo kulizua maswali kuhusu uwezekano wa gharama ya kuvunja mkataba.
Waziri wa Hazina ya Kitaifa John Mbadi mnamo Alhamisi alihakikishia Wakenya kuwa hakuna pesa zitakazopotea kutokana na kufutiliwa mbali kwa mkataba wa JKIA lakini hakusema hali itakavyokuwa katika kandarasi ya Ketraco.
“Mkataba wa Ketraco ulikuwa umepiga hatua na tutaangalia ikiwa kuna uwezekano wowote wa kugharamika. Walakini, kwa JKIA, hakuna pesa zilizopotea. Ulikuwa bado katika hatua za awali jinsi nilivyowaambia wabunge,” akasema Bw Mbadi.
Huku kiongozi wa nchi akichukua uamuzi huo wa kijasiri, maswali yaliibuliwa kuhusu uhusiano wa Adani Group katika mkataba wa Sh104 bilioni na Wizara ya Afya huku Dkt Ruto akikosa kuutaja katika hotuba yake.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba Apeiro Limited, yenye hisa nyingi zaidi katika muungano unaoongozwa na Safaricom ambao umepewa kandarasi ya mfumo wa teknolojia wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), ina uhusiano wa kibiashara na Kundi la Adani.
Serikali ilikabidhi muungano huo kandarasi ya kutoa Mfumo Shirikishi wa Teknolojia ya Huduma ya Afya (IHTS) kwa UHC.
Kila moja ya kampuni tatu itachangia katika Sh104.8 bilioni zinazohitajika kutekeleza, kudumisha na kustawisha mfumo wa IHTS katika kipindi cha miaka kumi ijayo kulingana na umiliki wao wa hisa.
Mbunge wa Seme, Dk James Nyikal, mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, alisema pamoja na kwamba ingawa kufutwa kwa mikataba chini ya Wizara ya Uchukuzi na Kawi ni jambo bora, kuna wasiwasi kwamba kiongozi wa nchi hakusema chochote kuhusu mpango huo wa Wizara ya Afya.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA