Matumaini ya kuondolewa ushuru wa nyumba yazimwa korti ikisema sheria iko sawa kabisa
MATUMAINI ya wafanyakazi nchini kupata afueni ya kuondolewa ushuru wa nyumba yalizimika jana baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa sheria ya ushuru huo imetimiza mahitaji yote ya kikatiba.
Mahakama ilitupilia mbali kesi sita zilizopipinga Sheria ya Nyumba Nafuu.
Jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliamua kuwa Sheria hiyo ilikidhi kiwango kinachohitajika cha ushirikishaji wa umma kabla ya kupitishwa Machi mwaka huu.
Majaji Olga Sewe, John Chigiti na Josephine Mong’are pia waliamua kwamba ushuru wa nyumba unaotozwa kwa kiwango cha asilimia 1.5 ya jumla ya mshahara wa kila mwezi wa mfanyakazi, ulipitishwa ipasavyo kwa mujibu wa katiba.
Wafanyakazi hukatwa asilimia 1.5 ya mshahara wao wote na hutumwa pamoja na mchango wa mwajiri wa asilimia sawa.
“Kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa na mzigo wa uthibitisho, tuliridhika kwamba kulikuwa na ushiriki wa kutosha wa umma kabla ya kupitishwa kwa Sheria,” walisema majaji.
Majaji hao pia walisema kwamba walalamishi waliopinga kutozwa kwa ushuru huo walikosa kuthibitisha kwamba ulikuwa wa kibaguzi na kubebesha mlipa ushuru mzigo wa ziada.
Dkt Magare Gikenyi na walalamishi wengine walikuwa wamedai kuwa ushuru huo ulikuwa wa kibaguzi kwani unalenga walioajiriwa rasmi huku wakiwatenga wanaojiajiri au wasio na ajira rasmi.
Majaji hao walisema ingawa serikali ilikiri kuwa ushiriki wa umma uliendeshwa katika kaunti 19, washikadau wakuu walialikwa kuwasilisha maoni yao mbele ya Bunge kupitia mawasilisho ya mdomo na maandishi.
Mahakama ilisema kwamba ingawa ushiriki wa umma ni muhimu, haimaanishi kwamba maoni yote lazima yazingatiwe.
“Swali ni ikiwa fursa ilitolewa kwa umma kutoa maoni yao,” walisema majaji na kuamua kuwa kuna ushahidi kwamba ushiriki wa kutosha wa umma ulifanywa kabla ya sheria kupitishwa.
Majaji hao pia walipuuzilia mbali madai kuwa serikali ya kitaifa inaingilia majukumu ya serikali za kaunti kwa kutaka kujenga nyumba kote nchini.
Walalamishi walidai kuwa jukumu la serikali ya kitaifa lilikuwa kuweka ajenda na uundaji wa sera.
Majaji, hata hivyo, walisema nyumba ni jukumu la pamoja na kwa kutekeleza jukumu hilo pamoja, ngazi zote mbili za serikali zilikuwa zikikuza kutegemeana.
Serikali ilitetea Sheria hiyo ikisema kwamba ushuru wa nyumba unakusudiwa kuwawezesha wananchi wote kuwa na uwezo sawa wa upatikanaji wa nyumba zenye staha na nafuu, kwa mujibu wa Kifungu cha 43 cha katiba.
Serikali pia ilisema ushuru wa nyumba nafuu umekitwa zaidi kwa wafanyikazi wanaolipwa mishahara na kujumuisha watu ambao wana vyanzo vingine vya mapato.
Majaji walisema kwamba hawakuona makosa katika uteuzi wa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) kama mkusanyaji wa mapato hayo, kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi.