Habari za Kitaifa

Mawakili: Agizo la Ruto makurutu wa NYS wapewe mafunzo ya bunduki ni ‘Hot Air’

Na JOSEPH OPENDA August 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AMRI ya Rais William Ruto kuwa vijana kwenye mafunzo ya Huduma za Kitaifa kwa Vijana (NYS) wafundishwe kutumia bunduki inaendelea kuzua maoni tofauti miongoni mwa Wakenya.

Rais William Ruto mnamo Jumatatu, Agosti 26, 2024 aliamrisha Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi akimtaka ashauriane na Wizara za Ulinzi na Usalama wa Ndani ili waibuke na mwongozo wa kuwafunza vijana wa NYS jinsi ya kutumia bunduki.

Akitoa amri hiyo wakati wa kufuzu kwa makurutu Gilgil, Kaunti ya Nakuru, Rais alisema mafunzo ya kutumia bunduki yatawezesha vijana hao kushiriki oparesheni za kijeshi katika maeneo mbalimbali nchini kukiwa na haja.

Hata hivyo, amri hiyo imepingwa na mawakili ambao wanasema Rais Ruto anastahili kukosolewa kwa kuwa matamshi yake hayazingatii sheria kwa msingi wa jinsi ambavyo idara za usalama huendesha shughuli zake.

Wakili Evans Ogada, anasema kuwapa vijana hao mafunzo ya kutumia bunduki kunaweza kusababisha kuchipuka kwa makundi ya wapiganaji nchini.

“Vijana 20,000 huchukuliwa na NYS kila mwaka na hata wakifunzwa matumizi ya bunduki si wote wataingizwa jeshi au katika idara ya polisi. Swali ni kipi kitafanyika na wale ambao wataachiliwa na hawana kazi?” akauliza Bw Ogada.

Kuhusiana na Katiba, Bw Ogada alisema jinsi ambavyo amri hiyo ilitolewa ni ishara tosha tu kuwa haina mashiko.

Anasema amri hiyo haina mashiko kwa kuwa lazima iandikwe rasmi lakini, hata hivyo, bado itakabiliwa na changamoto za kisheria.

Sheria inamhitaji rais apate idhini kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Usalama kabla ya kutoa matamshi kama hayo yanayohusiana na suala la usalama wa nchi.

Wakili Waikwa Wanyoike naye alisema kuwa Rais hana mamlaka ya kuamua kinachostahili kusheheni kwenye mafunzo ya NYS kwa kuwa jukumu hilo ni la mkurugenzi wa asasi hiyo.