Mawakili wakimbia kortini kuzuia Ruto asitie saini Mswada wa Fedha 2024
KUNDI la mawakili na wanaharakati wameelekea mahakamani kumzuia Rais William Ruto kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na Mswada wa Kibali cha Matumizi ya Fedha wa 2024.
Mawakili saba wakiwemo Ndegwa Njiru, Jackline Mwangi, Lempaa Suyinka na Chama cha Wanasheria wa Mlima Kenya wanataka mahakama itoe maagizo ya kumzuia Rais Ruto kutia saini mswada huo hadi kesi yao itakaposikizwa na kuamuliwa.
Mswada huo ulipitishwa katika Bunge la Kitaifa Jumanne licha ya maandamano ya kuupinga yaliyoshuhudiwa jijini Nairobi na kaunti zingine 36.
Kulingana na sheria, Rais Ruto anapaswa kutia saini Miswada hiyo kuwa sheria ndani ya siku 14 baaada ya kupitishwa kwayo.
Hata hivyo, anaweza kuikataa na kuirejesha Bungeni akiandamanisha na taarifa inayotaja sehemu ambazo angetaka zifanyiwe mabadiliko.
Ikiwa Dkt Ruto atadinda kushughulikia miswada hiyo miwili itakuwa sheria siku 14 baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa kuiwasilisha kwake.
Mwaka wa kifedha wa 2024/2025 unaanza Julai 1 na inatarajiwa kwamba serikali itakuwa ikikusanya ushuru chini ya mwongozo uliotolewa na Mswada wa Fedha wa 2024.
Katika kesi yao, mawakili hao wanadai kuwa mpango wa utayarishaji wa bajeti ulisheheni mabishano baada ya Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u kuwasilisha Bungeni Mswada wa Fedha wa 2024 mnamo Mei 9, 2024.
“Kwamba kwa mujibu wa Kipengele cha 222 (1) cha Katiba agizo litolewe la kumzuia Rais William Ruto kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na Mswada wa Matumizi ya Fedha za Bajeti ya 2024 kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii,” wakasema.
Kupitia wakili Kibe Mungai, watu hao wanasema kuwa maoni ya umma hayakushirikishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 inavyohitajika kulingana na kipengele cha 221 (2) cha Katiba.