Mawakili walivyokabana koo kesi ya Gachagua
JOTO la kutimuliwa mamlakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua liliwavuruga wengi kortini Jumanne huku mawakili wakikabana koo na hata kupelekea wakili mkongwe Dkt John Khaminwa kumkaripia mwanasheria mkuu wa zamani Profesa Githu Muigai kwamba alikuwa ‘ananyonya’ alipoanza kazi ya uanasheria.
Dkt Khaminwa ambaye amehudumu kama wakili wa mahakama kuu kwa takriban miaka 60 alimzomea Prof Muigai akimweleza hapasi kumwamuru akae kumruhusu Mwanasheria Mkuu Bi Dorcus Oduor kuwasilisha tetezi zake katika kesi za kupinga kutimuliwa kazini kwa Bw Gachagua.
Wakili huyo mkongwe alipandwa na mori kupaaza sauti na kumweleza Prof Muigai, “hupasi kuniamuru nikae. Nikianza kazi ya uwakili ulikuwa unanyonya. Lazima hii mahakama itathmini utaratibu wa kuwateua majaji hawa watatu wanaosikiza kesi za kupinga uteuzi wa Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.”
Dkt Khaminwa alisema kwamba uteuzi wa Majaji Eric Ogola, Antony Mrima na Freda Mugambi haukuambatana na sheria na kwamba “hawapasi kusikiza kesi hiyo.”
Wakili huyo alichemka kwa hasira huku akiomba mahakama isikubalie kutumika vibaya.
Ni wakati huo Prof Muigai alisimama kwa uadilifu na upole na kuomba ufafanuzi wa kesi inayojadiliwa ndipo ajue masuala atakayojibu.
Prof Muigai aliyeteuliwa kumtetea Mwanasheria Mkuu Bi Dorcus Oduor aliyeshtakiwa pamoja na Rais William Ruto, Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki, Maspika wa mabunge yote- Bunge la Kitaifa na Seneti –Mabw Moses Wetang’ula na Amason Kingi mtawalia alisema “ni jambo la busara kujua kesi wanayoendelea nayo ndipo ajue atakavyojibu.”
Wakati huo Dkt Khaminwa alikuwa anamtazama kwa ukali huku akizugumza wakati mmoja naye.
“Naomba Dkt Khaminwa uketi. Mwongozo bora ni kwamba Mwanasheria Mkuu ndiye kiongozi wa mawakili wote na anapozugumza kila wakili mwingine yeyote anatakiwa kunyamaza.”
Matamshi hayo yalimuudhi Dkt Khaminwa ndipo akajibu kwa ukali “Huwezi kuniamuru niketi. Mawakili wengine hapa wanajiita Maprofesa wa Sheria na wataalam washeria. Wao hawajui. Nikianza uanasheria ulikuwa unanyonya tu.”
Dkt Khaminwa alisema hakuna haraka ya kusikiza kesi hiyo. Alishangaa mbona serikali inaharakisha kusikizwa kwa kesi ya kuapishwa kwa Prof Kindiki.
“Tuko na haraka ya kwenda wapi. Bunge lilipitisha kwa haraka na kinyume cha sheria kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua na sasa Jaji Mwilu aliamuru kesi ya kuapishwa kwa Prof Kindiki isikizwe kwa haraka. Tuko na haraka ya kwenda wapi,” Dkt Khaminwa alishangaa.
Aliendelea kusema kwamba Kenya imeorodheshwa kuwa moja ya nchi fisadi ulimwenguni na kutahadharisha mahakama isiwe na pupa ya kusikiza na kuamua kesi za kutimuliwa kwa Bw Gachagua la sivyo idara ya mahakama na majaji wataonekana kuwa wafisadi pia.
Prof Muigai alisimama kidete na kueleza mahakama lazima kuwe na utaratibu na lazima mawakili wajadilie hoja za kesi ambayo mwanasheria mkuu na mawakili wengine wanapasa kujibu.
Hasira zilitulia ndipo Dkt Khaminwa akakaa na kesi ikaendelea.
Prof Muigai alitetea uteuzi wa Majaji Ogola, Mrima na Mugambi na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu akisema hakukaidi sheria kuwateua majaji hao kusikiza kesi ya kutimuliwa mamlakani kwa Bw Gachagua na kuteuliwa kwa Prof Kindiki.
Hata hivyo joto la kufukuzwa kazini halikutulia ila iliendelea kuwavuruga mawakili wengine.
Mawakili Njiru Ndegwa, Kibe Mungai na wakili mwenye tajriba ya juu Paul Muite wanaomtetea Bw Gachagua na Bw Munyi Mathenge walikabana koo na mawakili wanaowakilisha mabunge Paul Nyamondi, Peter Wanyama, Ben Millimo na Dkt Adrian Kamotho anayewakilisha Rais William Ruto.
Mawakili wa upande wa Bw Gachagua walidai Jaji Mwilu hana mamlaka ya kuwateua majaji kusikiza kesi ya kufukuzwa kazi kwa Naibu Rais.
Mabw Muite, Mungai, Njiru na Profesa Elisha Ongoya walidai Kifungu nambari 163 (4) cha Katiba hakimruhusu Naibu Jaji Mkuu kuteua majaji kusikiza kesi yoyote ya ufafanuzi wa sheria.
Mawakili hao walidai Jaji Mwilu aliendea faili ya kusimamisha uteuzi wa Prof Kindiki kutwaa wadhifa wa Naibu Rais usiku wa Ijumaa na kuamuru Majaji Ogola, Mrima na Mugambi kukaa siku ya Jumamosi Oktoba 19, 2024.
“Jaji Mwilu alitoa maagizo usiku wa Oktoba 18, 2024 kesi ya mwanasheria mkuu ya kufutiliwa mbali uteuzi wa Prof Kindiki isikizwe. Aliwateua kinyume cha sheria majaji watatu kusikiza ombi la mwanasheria mkuu,” Bw Muite alisema.
Hasira ya Dkt Khaminwa iliwaka ndipo akidai “uteuzi wa jopo la majaji watatu kusikiza ombi la kufutilia mbali agizo la kuzima kuapishwa kwa Prof Kindiki Bw Gachagua”
Mawakili walikwaruzana kisheria huku kila upande ukivuta ngozi ya haki upande wao.
Mawakili wa serikali waliomba mahakama itupilie mbali ombi la Bw Muite na wenzake kwamba majaji hao wakome kusikiza kesi hiyo na wairudishe faili kwa Jaji Mkuu Martha Koome kuteua jopo lingine.
Profesa Tom Ojienda anayewakilisha bunge la Seneti katika kesi hiyo alisema kwamba uamuzi wa mabunge yote ulitamatisha kazi ya Bw Gachagua.
“Hakuna uamuzi wowote wa mahakama unaweza kubatilisha uamuzi wa bunge la Seneti kwamba Bw Gachagua hafai kuhudumu kama Naibu Rais.Alipatikana na hatia ya kueneza ukabila na ufisadi. Uamuzi wa Seneti ndio wa mwisho,” Prof Ojienda alisema.
Prof Ojienda alimtetea Jaji Mwilu dhidi ya madai alikosea kuwateua majaji hao watatu kusikiza kesi la mwanasheria mkuu kuu kuruhusu Prof Kindiki aapishwe.
Alisema Jaji Koome alikuwa safarini nchini Geneva na kwamba akienda alikuwa amempa mamlaka Jaji Mwilu kuendeleza idara ya mahakama na kutekeleza majukumu yake.
Prof Ojienda aliomba mahakama itupilie mbali ombi la Bw Gachagua la kutaka Majaji Ogolla, Mrima na Mugambi wakome kusikiza kesi hiyo kwa madai waliteuliwa kwa njia isiyopasa na Jaji Mwilu.
Mahakama hata hivyo Jumatano Oktoba 23, 2024 ilitoa uamuzi kwamba Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakukosea kuunda jopo na kwamba jopo lipo kazini kisheria.