Mawakili zaidi ya 200 katika afisi ya AG kusubiri zaidi kupandishwa vyeo
ZAIDI ya mawakili 200 katika afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliofaa kupandishwa vyeo mwaka jana, 2024, wataendelea kusubiri hadi kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya Ajira na Masuala ya Leba iamuliwe.
Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba maslahi ya umma yangetekelezwa vyema kwa kusitisha mpango huo hadi mahakama itakapoamua iwapo hatua hiyo ilifuata sheria.
Majaji Daniel Musinga, Francis Tuiyott na George Odunga, walisema kwamba hasara yoyote mawakili 212 wa serikali walipata, inaweza kulipwa ikiwa kesi ya kupinga kupandishwa cheo itatupiliwa mbali.
“Tunatupilia mbali notisi ya ombi la Desemba 11, 2024,” mahakama ilisema.
Afisi ya Mwanasheria Mkuu ilikimbilia kortini mwaka jana, baada ya Hakimu Byram Ongaya, kusimamisha hatua hiyo hadi kuamuliwa kwa ombi lililowasilishwa na Dkt Benjamin Magare-Gikenyi, Dishon Mogire na Philemon Abuga.
Dkt Gikenyi alidokeza kuwa kati ya nyadhifa 15 kuu zilizotolewa Novemba 26 mwaka jana, watu tisa walikuwa wa kabila moja huku 12 wakiwa wanawake.
Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) iliunga mkono kesi hiyo, ikisema kwamba upandishaji vyeo ulifanywa kwa ukiukaji mkubwa wa Katiba, Sheria ya Utumishi wa Umma, afisi ya Sheria ya Mwanasheria Mkuu na mwongozo wa sera na taratibu zinazohitajika.
“Tume inaunga mkono ombi hilo kikamilifu na kwa unyenyekevu kuitaka mahakama hii tukufu kutoa misaada yote iliyomo kama ilivyoainishwa,” PSC ilisema.
Bw John Kimani, mkurugenzi katika PSC, alisema ni lazima maafisa wote wa umma wapewe fursa sawa ili kutuma maombi yao.
Nafasi ambazo zilisitishwa ni za manaibu wawili wa mawakili wakuu, manaibu wa wakili mkuu (nafasi 13), mawakili wanne wa serikali, naibu wakili mkuu wa serikali (nafasi 63) na mawakili 145 wa serikali.
Alipokuwa akitetea upandishwaji wa vyeo, Bw Oscar Eredi, alisema zoezi hilo lilifanyika kwa utaratibu uliofaa kisheria.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali alianza mchakato wa utekelezaji wa Sheria kulingana na marekebisho ambayo yamefanywa,” Wakili Mkuu Shadrack Mose alisema katika hati ya kiapo.
Bw Mose aliongeza kuwa mojawapo ya michakato hiyo ni uhakiki wa idadi ya wafanyikazi ili kuwezesha afisi hiyo kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na pia kutoa huduma kwa Wakenya ipasavyo.
Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor akihutubia wanahabari wakati wa kuzindua kituo cha stakabadhi ukanda wa Kisumu katika Haki Building, Februari 5, 2025. Afisi hiyo inagatua huduma zake kwa kaunti zote 47. PICHA|MAKTABA