Habari za Kitaifa

Mazoezi ya KCSE kuendelea ilivyopangwa Ijumaa licha ya kutangazwa Siku Kuu

Na LYNET IGADWAH October 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Elimu imethibitisha kuwa mazoezi ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) yataendelea kama kawaida leo, Ijumaa, Oktoba 17, 2025 licha ya serikali kutangaza siku hiyo kuwa ya mapumziko ya kitaifa.

Ijumaa imetangazwa kuwa siku ya mapumziko kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Amolo Odinga, aliyefariki dunia Jumatano asubuhi akiwa nchini India, akiwa na umri wa miaka 80.

Maafisa wa juu kutoka Wizara ya Elimu wamesema kuwa mazoezi haya hayawezi kuahirishwa kwani kufanya hivyo kutasababisha mabadiliko yasiyotarajiwa katika ratiba rasmi ya mitihani ya kitaifa.

“Kwa kawaida, mazoezi haya hayaingiliwi kwa namna yoyote. Maafisa walio mashinani tayari wameelekezwa na wanafahamu watakachofanya,” alisema afisa mmoja mkuu kutoka wizara hiyo.

Wakati wa mazoezi haya, watahiniwa huelekezwa kuhusu taratibu na kanuni za mitihani zilizowekwa na Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC), ikiwa ni pamoja na maadili yanayotarajiwa, usimamizi wa muda, na orodha ya vitu vinavyoruhusiwa na visivyoruhusiwa katika chumba cha mtihani.

Kwa upande wao, walimu na wasimamizi wa mitihani hupitia tena mwongozo wa usimamizi wa mtihani, usalama wa vifaa vya mitihani, na njia za kuhakikisha uadilifu wa mitihani unaendelea kudumishwa.

Mtihani wa KCSE utaanza rasmi Oktoba 21, 2025. Watahiniwa wataanza na mitihani ya masomo ya lugha za Kifaransa, Kijerumani, Kiarabu, na Lugha ya Ishara ya Kenya.

Wizara ya Elimu imetoa wito kwa wanafunzi, walimu, na wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanahudhuria mazoezi hayo kwa sababu ni hatua muhimu ya maandalizi kabla ya kuanza kwa mitihani rasmi.