Habari za Kitaifa

Mbadi apendelea maafisa wakuu kwa kuwaondolea ushuru wa posho

Na Vincent Owino May 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI wa kipato cha juu wanaosafiri mara kwa mara kikazi wanatarajiwa kufaidika kutokana na msamaha wa ushuru katika Mswada wa Fedha wa mwaka 2025, unaopendekeza kuongeza posho ya kila siku isiyotozwa ushuru kutoka Sh 2,000 hadi Sh 10,000.

Ongezeko hilo la mara tano linawapendelea hasa maafisa wakuu wa serikali na wakurugenzi wa mashirika ya kibinafsi ambao hupokea viwango vya juu vya posho za kila siku wanaposafiri kikazi ndani na nje ya nchi.

Posho la kila siku ni fedha zinazotolewa kwa wafanyakazi kufidia gharama kama chakula, malazi na usafiri wa ndani wanapokuwa katika safari ya kikazi mbali na maeneo yao ya kawaida ya kazi.

“Kifungu cha 5 cha Sheria ya Ushuru wa Mapato kinarekebishwa katika kipengele cha (iii) cha kifungu kidogo (2)(a) kwa kufuta maneno ‘shilingi elfu mbili’ na badala yake kuweka maneno ‘shilingi elfu kumi’,” unasema Mswada huo.

Chini ya mfumo wa sasa wa ushuru, ni Sh2,000 tu za kwanza kutoka kwa posho ya kila siku ambazo hazitozwi kodi. Pendekezo jipya linamaanisha kuwa wafanyakazi watakaopokea hadi Sh10,000 kwa siku hawatatozwa ushuru kwa posho hiyo, huku wanaopokea zaidi ya kiwango hicho wakitozwa kwa kiasi kinachozidi Sh10,000.

Pendekezo hili linafanana na lile lililokuwa kwenye Mswada wa Fedha wa mwaka jana ambao Rais William Ruto aliuondoa kufuatia maandamano dhidi ya mapendekezo ya kuongeza mapato ya serikali yaliyokuwemo kwenye mswada huo.

Mswada huo wa mwaka jana uliopingwa vikali ulikuwa unapendekeza kwamba posho ya kila siku inayotozwa kodi iwe inayozidi asilimia tano ya mshahara wa mwezi wa mfanyakazi, badala ya kiwango cha Sh2,000.

Maafisa wakuu wa serikali huwa wanapokea kiasi kikubwa zaidi cha posho, jambo linalodhihirika kupitia ripoti za Matumizi ya Bajeti kutoka kwa Mdhibiti wa Bajeti, ambazo huonyesha matumizi makubwa katika safari za ndani na za kimataifa.

Kwa mfano, kulingana na data kutoka Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), Waziri anaweza kulipwa hadi Sh194,550 kama posho ya kila siku anapotembelea nchi kama Singapore.

Matumizi ya serikali katika safari za ndani na nje ya nchi yamekuwa yakimeza sehemu kubwa ya bajeti za wizara mbalimbali, huku ofisi kama ya Rais, Naibu Rais na Mkuu wa Mawaziri zikiongoza kwa matumizi hayo.

Katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2024, serikali ilitumia Sh6.5 bilioni kwa safari za ndani na Sh3.1 bilioni kwa safari za nje ya nchi, ambapo sehemu kubwa ya matumizi hayo yalikuwa ni kulipa posho za kila siku.