Habari za Kitaifa

Mbona ulisubiri sana? Gen Z wambana Ruto huku akiahidi kufanya mageuzi


RAIS William Ruto ameonekana kukubali matakwa ya vijana walioandamana dhidi ya serikali yake kwa kuchukua hatua za kupunguza gharama ya maisha ikiwa ni pamoja na kufuta ofisi za mke wake, mke wa naibu rais na mkuu wa mawaziri.

Rais pia alitangaza kuwa atafanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri akisema amesikia malalamishi ya vijana.

Hata hivyo, Rais alikataa wito wa Wakenya kuwafuta kazi mawaziri wake wote na kuteua wapya akisema ana mipango tofauti.

Miongoni mwa matakwa ya vijana walioandamana kwa majuma matatu ilikuwa ni raia kuwatimua mawaziri wote waliotajwa kuhusika katika ufisadi na kujilimbikizia utajiri wa haraka.

Kulikuwa na ripoti kwamba Rais angewatimua mawaziri baada ya kusema alikuwa amesikia sauti za vijana na kuwaita kwa kikao katika mtandao wa X spaces jana.

Hata hivyo, akizungumza moja kwa moja na vijana katika kikao hicho, kiongozi wa nchi alipuuza wito huo akisema amepanga hatua kadhaa kushughulikia masuala ambayo yamepaka tope baraza lake la mawaziri.

“Sitalivunja Baraza la Mawaziri kwa sababu niko katika harakati za kuangalia mambo kwa njia tofauti,” Rais Ruto alisema.

Hata hivyo, Rais Ruto aliwaonya mawaziri dhidi ya kujihusisha na ufisadi na kusema kuwa yuko tayari kumfuta kazi waziri wa aina hiyo.

“Sitasita kumfuta kazi waziri yeyote atakayefikishwa kortini kukiwa na ushahidi kwamba alihusika katika ufisadi,” alisema kiongozi wa nchi.

Ruto aliomba Wakenya msamaha kutokana na malalamishi kwamba baadhi ya wanasiasa waliochaguliwa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) walikuwa na kiburi kwa Wakenya.

Hasa, aliomba msamaha kwa niaba ya mbunge wa Molo Kuria Kimani na mwenzake wa Kikuyu Kimani Ichung’wah ambao walitoa matamshi ambayo hayakufurahisha umma.

Kabla ya kikao cha jana, Rais William Ruto alitangaza hatua kadhaa za kupunguza matumizi ya serikali baada ya kukataa Mswada wa Fedha 2024 ikiwemo kupiga marufuku harambee ambazo wanasiasa wamekuwa wakitumia kujipigia debe.

Rais alimwagiza Mwanasheria Mkuu Justin Muturi kutayarisha sheria na kuunda utaratibu wa michango ya wazi kwa lengo la kutoa misaada hasa kwa matibabu.

“Naagiza Mwanasheria Mkuu kuandaa na kuwasilisha sheria kufafanua utaratibu uliopangwa na wa wazi wa michango ya umma,” alisema.

Kwa kufanya hivyo, alipiga marufuku watumishi wa umma kushiriki katika harambee.

“Hakuna afisa wa serikali atakayehitajika kushiriki katika kuchangisha pesa za umma katika harambee,” Rais Ruto alisema.

Maafisa wa serikali na watumishi wa umma wamekuwa wakimulikwa kwa kutoa mamilioni ya pesa makanisani na katika hafla mbalimbali za kuchangisha pesa.

Katika hatua ya kupunguza matumizi, Rais William Ruto ametangaza kwamba atapunguza idadi ya washauri wa serikali hadi nusu.

Uamuzi huu unalenga kuongeza ufanisi ndani ya utumishi wa umma na unapaswa kutekelezwa mara moja.

“Idadi ya washauri katika serikali itapunguzwa kwa asilimia 50 mara moja,” Rais Ruto alisema wakati wa hotuba yake kwa Taifa.

Kupunguzwa huku ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa Rais wa kuondoa matumizi yasiyo ya lazima ya serikali na kuboresha utoaji wa huduma.

Mbali na kupunguza idadi ya washauri, Rais Ruto alizindua mpango wa kufuta mashirika 47 ya serikali ambayo yana majukumu yanayofanana.

Alisema watumishi hao kutoka katika mashirika hayo watapewa kazi nyingine katika wizara na idara mbalimbali ndani ya serikali.

“Mashirika arobaini na saba yenye kazi zinazofanana yatavunjwa, na hivyo kusababisha kuondolewa kwa gharama zao za uendeshaji. Kazi zao zitaunganishwa katika wizara husika,” Ruto alieleza.

Hatua hii inalenga kuondoa gharama, kurahisisha utendakazi wa serikali na kuimarisha uratibu ndani ya utumishi wa umma.

Rais pia alisimamisha ununuzi wa magari mapya serikalini kwa muda wa miezi 12, isipokuwa kwa idara za usalama na akaweka mikakati ya kuokoa pesa kuajiri walimu wa JSS na madaktari wanagenzi.

Rais William Ruto pia alisimamisha safari zisizo za lazima kwa wafanyakazi wa serikali ndani na nje ya nchi.