Mbunge adhalilisha Kalonzo, asema hatoshi mboga mbele ya Ruto 2027
MBUNGE wa Saboti, Caleb Amisi, amemkejeli Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na wandani wake kwenye upinzani, akisema hawajaiva ya kutosha kumng’oa mamlakani Rais William Ruto mnamo 2027.
Bw Amisi amesema kuwa siasa za Bw Musyoka na baadhi ya viongozi anaoandamana nao kama vile Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa na Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinard Waititu haziwezi kumpelekea kokote.
Alisema wanasiasa hao hawana nguvu au umaarufu wowote ambao unaweza kumsaidia Bw Musyoka kumwangusha Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ni ukweli kuwa watu hawapendi Ruto lakini tuambiane ukweli, hawa watu kama Kalonzo na walioko hapa ndio watatoa Ruto? Mimi siwezi kudanganya mchana, Waititu ndiye anaweza kupeleka Kalonzo kwa Mlima ambao sasa umeteremka?” akahoji Bw Amisi.
Alikuwa akihutubu katika mazishi ya Josiah Marende, babake Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa, Kenneth Otiato Marende, katika eneobunge la Luanda, Kaunti ya Vihiga. Bw Marende alihudumu kama Spika kati ya 2007-2013 wakati wa serikali ya Muungano.
Bw Musyoka, Jeremiah Kioni, Eugene Wamalwa na Waititu na viongozi wengine walihudhuria mazishi hayo na walitazama tu huku Bw Amisi, mbunge wa ODM akiwachemsha vijana na kushangiliwa na umati wakati alikuwa akiwavamia kwa maneno makali.
Waziri wa Vyama vya Ushirika na Vyama Vidogo Wycliffe Oparanya na Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi pia walihudhuria mazishi hayo yaliyosheheni cheche kali za kisiasa.
“Watu hawapendi Ruto na hata mimi najua hivyo lakini ambieni Kalonzo atoe meno nje, aume watu meno tuone. Hata kama anaogopa, arushe hata mawe kwenye kituo cha polisi ashikwe aende ndani.”
“Kutembea kwa matanga eti unataka kuwa rais wa Kenya hakutakufaa kitu. Hata Donald Trump Rais wa Amerika ana kesi ngapi kwa mahakama? Rais wa Botswana na Senegal walitoka jela wakaenda kuwa marais.”
“Watu wanamtaka mtu ambaye anaweza kujinyima na kuwapigania lakini si hizi siasa za Kalonzo na wenzake,” akakejeli Bw Amisi.
Bw Amisi ni kati ya viongozi waliovuna kwenye mabadiliko yaliyotekelezwa na ODM bungeni baada ya kuteuliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC).
Hii ni kufuatia kuteuliwa kwa baadhi ya wanachama wakuu wa ODM kuwa mawaziri serikalini.
Bw Waititu alimjibu mbunge huyo na kusema kuwa ni Bw Musyoka pekee ndiye anatosha kuwa rais mnamo 2027 kwa kuwa alifanya kazi pamoja na Rais Mwai Kibaki na kusaidia kuinua uchumi wa nchi.
“Watu wa Magharibi mnastahili kugutuka kwa sababu sisi tulidanganywa mlimani na sasa tumeondoka UDA. Ifikiapo 2027, Rais atakuwa Bw Kalonzo akisaidiwa na Wamalwa,” akasema Bw Waititu.
Bw Musyoka aliposimama aliwakashifu viongozi wa ODM walioingia serikalini na kusema kuwa wimbi la mabadiliko ambalo linashuhudiwa Afrika, litatua hata hapa nchini.
Alisema kuwa ataendelea kukaa ngumu kwenye upinzani na anatosha kuwa rais 2027 hata akisawiriwa vibaya na maadui wake.