Habari za Kitaifa

Mbunge Mwengi Mutuse ashikilia atapeleka Bungeni hoja ya kutimua Gachagua Jumanne alasiri

Na  CHARLES WASONGA October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Kibwezi Mashariki Mwengi Mutuse amethibitisha kuwa ndiye mdhamini wa hoja ya kumtimua afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hii ni baada ya wanahabari kupata nakala ya hoja hiyo ambayo imeelezea kwa kina tuhuma tatu kuu dhidi ya Bw Gachagua ambazo ni; Ukiukaji wa Katiba na sheria nyinginezo, ukiukaji wa sheria za kitaifa na kimataifa na utovu wa maadili.

“Ndio nakala hiyo ni halali na ndimi mdhamini wa hoja hiyo. Nitaitetea rasmi bunge leo (Jumanne) katika kikao cha alasiri,” akasema Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya Chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC).

“Mengi yatajitokeza baadaye,” akaongeza.

Kwa mfano, kulingana na hoja hiyo, Bw Mutuse anamtuhumu Bw Gachagua kwa ukiukaji wa vipengele vya 10, 27, 73, 75 na 129 vya Katiba ya sasa kwa kueneza ukabila, ubaguzi na kusababisha migawanyiko kitaifa.

“Kwa mfano wakati mmoja mnamo 2023 katika mkutano wa hadhara katika kaunti ya Kajiado, Naibu Rais alitoa matamshi ya kuchochezi kwamba Serikali ya Kenya ni Kampuni na kwamba ugavi wa miradi ya maendeleo na rasilimali ya umma inapasa kufanywa kwa misingi ya ‘hisa’ inayokadiriwa kutokana na jinsi watu kutoka jamii mbalimbali walipiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2022. Kauli kama hii inaendeleza ukabila, ubaguzi na kuvunja utaifa,” anasema katika hoja hiyo.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba hoja hiyo tayari imepata uungwaji mkono kutoka zaidi ya wabunge 300, kutoka mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio.

Hata hivyo, nakala ya hoja ambayo Taifa Dijitali imepata haina orodha ya wabunge wanaoinga mkono.

Kwa mujibu wa Kipengele cha 150 cha Katiba hoja ya kumtimua Naibu Rais inapasa kuungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge wote, kabla ya Spika wa Bunge la Kitaifa kuruhusu ijadiliwe. Hiyo ni sawa na wabunge 117 kati ya 349.

Aidha, inapasa kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya wabunge wote (yaani wabunge 233) ili ipitishwe kwa Seneti ambako pia itahitaji kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya maseneta (sawa na maseneta 45 kati ya 67).