Habari za Kitaifa

Migawanyiko yazidi mlimani Gachagua akilaumiwa kwa Raila kuingia Serikalini

Na MWANGI MUIRURI July 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIGAWANYIKO ya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya iliendelea kushika kasi Alhamisi,  huku Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, akimshutumu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumhangaisha Rais William Ruto, hadi akalazimika kumwendea Raila Odinga kuleta utulivu serikalini.

Bw Kiunjuri ambaye ni kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) kinachounga Kenya Kwanza, alisema Bw Gachagua anawajibika kikamilifu kwa serikali ya muungano wa kitaifa ambayo ilitajwa Jumatano, ambapo washirika wanne wa Bw Odinga waliteuliwa mawaziri.

“Tulimtuma mtu kwenye meza ya chakula lakini alianza kazi ya kulia zaidi hata wakati mdomo wake ulikuwa umejaa chakula na hivyo kutuonyesha sisi kama watu walafi ambao ni vigumu kufurahishwa,” akasema Bw Kiunjuri.

Haya yalijiri huku wakili Bw Ahmednasir Abdullahi, akisema kuingia kwa washirika wa Bw Odinga serikalini, kunamaanisha Bw Gachagua ameisha kisiasa.

“Bw Gachagua ndiye amepoteza pakubwa zaidi katika baraza la mawaziri na serikali iliyobuniwa upya. Yeye ni mfu anayetembea. Ni mwanasiasa aliyejeruhiwa vibaya na nadhani atakufa kwa majeraha yake kabla ya 2027,” akasema.

Aliongeza “Ingawa asilimia 37 ya baraza la mawaziri wanatoka eneo la Mlima Kenya, hakuna hata mmoja anayedai kuwa mwaminifu kwake.”

Lakini aliyekuwa mgombea wa Urais, Bw Peter Kenneth, alisema kuwa maadamu Bw Gachagua yuko afisini, hawezi kudharauliwa kwani lolote linaweza kutokea na kujipata kwenye usukani.

Bw Kenneth alisema juhudi za Bw Gachagua kubadilika na kupanga siasa zake ili kuweza kubaini umuhimu wa uwiano wa kitaifa, hazifai kupuuzwa.

Kwa upande wake, Bw Kiunjuri aliongeza, “Mlima Kenya inastahili kujilaumu kupitia Bw Gachagua kwa kutonyenyekea ndani ya serikali ambayo tulikuwa na hisia nyingi.”

Alidai Mlima Kenya kupitia njama iliyobuniwa na wanasiasa wanne kwa ushirikiano na wengine wawili kutoka Azimio, ilifadhili wahuni 35,000 kuvuruga maandamano ya amani ya Gen Z ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 katika nia ya kumwondoa Rais Ruto mamlakani.

“Rais ametufichua baadhi yetu na wengine tayari wamerekodi taarifa kwa polisi. Tunajua ni nani na nani walihusika katika njama hiyo, tuna ushahidi wa sauti na eksibiti pamoja na jinsi pesa zilitolewa,” akasema.

Bw Kiunjuri aliongeza “Mmoja wa viongozi wetu wakuu kutoka eneo la Mlima Kenya alifadhili baadhi ya wahuni na kwa mfano, eneo bunge la Juja pekee lilituma watu 3,000 katika maandamano ambayo yaliishia kuvamia na kuchoma sehemu ya Bunge la Kitaifa.

“Wenzetu wanne waliungana na wengine wawili wa Nairobi. Tuna wale ambao viongozi wetu walafi wamekuwa wakiwaandaa ili kuchukua kiti cha ugavana wa Nairobi. Mlima Kenya ulifadhili watu 25,000, wale wa Azimio walifadhili 10,000 na hivi karibuni watajulikana,” akasema.

“Huenda sasa tunaendeleza siasa nyingi zinazotegemea maslahi ya kibinafsi badala ya manufaa ya wote,” akasema aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi.