Habari za Kitaifa

Mjadala wa AUC: Raila Odinga ametosha unga kuwa mwenyekiti?

Na DANIEL OGETTA December 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MDAHALO kuhusu uwaniaji wa mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AUC) uliofanyika Ijumaa, Desemba 13, 2024 ambapo kinara wa ODM, Raila Odinga, alikabiliana ana kwa ana na wagombea wenzake, umeibua hisia mseto miongoni mwa wakenya.

Wafuasi wa dhati wa Bw Odinga wanaamini “alishinda mdahalo huo kwa mbali” huku wakosoaji wa aliyekuwa Waziri Mkuu wakiendelea kupuuzilia mbali azma yake.

Profesa Makau Mutua aliye katika timu ya kampeni ya Bw Odinga amesisitiza kuwa kinara wa ODM atakuwa tayari siku ya kwanza kufanyia Afrika kazi.

“Pongezi Raila Odinga. Mdahalo wa kufana na ishara ya uongozi kwa Afrika,” alisema Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi.

AUC inahitaji kiongozi anayeweza kuunganisha Afrika kwa lengo moja na kuimarisha raslimali tele za bara hili ikiwemo wafanyakazi, alisema Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Korir Sing’oei.

“Raila Odinga amesheheni tajriba ya kipekee na sifa ya kumwezesha kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC),” alifafanua Bw Korir.

Kauli yake ilirejelewa na mtaalam wa mikakati ya kisiasa, Pauline Njoroge: “Kile ambacho AUC inahitaji kwa sasa ni mwanasiasa mwenye tajriba na maono, sio tu kiongozi atakayevutia watu bila umaarufu wa kuunganisha, kupatanisha na hata kukusanya viongozi wa mataifa na wadau wakuu kuchukua hatua. Raila Odinga amethibitisha kuwa na sifa zinazohitajika.”

Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, ambaye alikuwa kinara wa ODM na aliyekabidhdiwa jukumu la kushikilia chama hicho kwa muda huu, alisema Bw Odinga “alijibu maswali kwa utulivu na kusudi imara.”

Bw Nyong’o alisema amewasiliana na wasomi wenzake kutoka sehemu mbalimbali Afrika waliotazama mdahalo huo ulioshirikisha wagombea watatu wanaomezea mate wadhifa wa AUC na kauli yao “inaonekana kuwa wazi – Raila Amolo Odinga alifanya vyema zaidi kuliko wawaniaji hao wengine wawili ambao pia walijitahidi.”

Mkurugenzi wa Biashara na Utalii Somaliland, Abdirashid Ibrahim, Bw Odinga “alifanya vyema katika Mjadala Afrika, na kuonyesha maarifa kihistoria na ujuzi wa kipekee.”

Hata hivyo, mwanasiasa Kabando wa Kabando, ana maoni tofauti.

“Nimempigia kura Raila Odinga kuwa rais wa Kenya mara mbili kwa ari (2022), na kisiri (2017). Kura yangu ya kwanza kwa urais nilimpigiua Jaramogi Oginga (1992). Lakini leo, 2024, naomba Raila ashindwe,” alisema Bw Kabando.

Bw Odinga alikabiliana katika mdahalo huo na Waziri wa Masuala ya Kigeni Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf, na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Madagascar, Richard James Randriamandrato.

Imetafsiriwa na Mary Wangari