Habari za Kitaifa

Mkengeuko Gachagua sasa akidai hazina ya fedha haikuwa tupu 2022

Na CECIL ODONGO May 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amepiga abautani na kudai kwamba Kenya Kwanza haikurithi hazina tupu walipochukua mamlaka baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa kiasi fulani tulipata hazina tupu lakini kulikuwa na pesa za kutosha kuhakikisha kwamba taifa linaanza kupiga hatua na kusonga mbele. Hakukuwa na pesa nyingi lakini kulikuwa na pesa za kutosha kusaidia uchumi wa Kenya kuwa thabiti,” akasema Bw Gachagua.

Alikuwa akiongea mnamo Ijumaa kwenye mahojiano na mwanahabari Oga Obinna ambapo alifichua jinsi Rais William Ruto alivyofika nyumbani kwake na kumlilia ili amuunge mkono 2022.

Kauli yake inakinzana na madai yake ya  hapo awali kuwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulipora pesa zote na kuacha hazina kuu ikiwa bila chochote mnamo 2022.

“Ukweli wa mambo ni kuwa tumerithi uchumi ambao unaelekea kuporomoka na kusababisha utoaji wa huduma kwa Wakenya kusitishwa. Tuna kazi kubwa kuhakikisha kwamba tunakomboa taifa hili na kulirejesha mahali ambapo Kibaki aliliacha,” akasema Bw Gachagua mnamo Septemba 13, 2022.

“Kwenye hazina kuu hakuna kitu, i tupu. Lazima tuanze bila kitu,” akasema wakati wa kuapishwa kwao katika uwanja wa Kasarani huku akishangaza hata wageni waalikwa ambao walikuwepo.

Kwa wakati mmoja, Bw Gachagua alisema kwamba hawakupata hata ‘panya’ kwenye hazina ya taifa, kauli ambayo iliashiria kuwa hali ilikuwa mbaya zaidi kiuchumi nchini.

Haijulikani jinsi ambavyo Bw Gachagua amebadili msimamo lakini inaonekana kuwa huenda kukosana kwake na Rais Ruto ndiko kumechangia msimamo huo.

Wakati wa mahojiana hayo, Bw Gachagua alisema kuwa ndiye alikuwa na ujasiri wa kumkabili Rais na akajuta kwa nini alimtoroka Bw Kenyatta kisha kuunga William Ruto 2022.

“Huyu ni mtu mkubwa wa zaidi ya miaka 50 na alikuwa akilia nyumbani kwangu eti nisimtoroke. Nilishangaa na hata nikaambia mchungaji (mkewe Dorcas) tumsikilize, tumwamini na kufanya kazi naye kuelekea uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Gachagua.

Naibu huyo wa rais wa zamani alisema kwamba utawala wa sasa hautaleta mabadiliko yoyote kwa sababu shida kuu ni Rais Ruto mwenyewe.

“Rais Ruto ana washauri lakini yeye ndiye huwashauri. Mambo yataendelea kuwa hata mabaya zaidi kabla ya 2027. Rais ni mwongo na hata baada ya kuwatimua mawaziri 13 tangu aingie madarakani, bado hakuna chochote ambacho kimebadilika serikalini,” akasema.

Naibu huyo wa rais wa zamani ambaye alibanduliwa mamlakani mnamo Oktoba mwaka jana, alijuta kuunga Rais Ruto na kusema kwa sasa atashirikiana na viongozi wengine kubadilisha nchi hii mnamo 2027.

Alidai kwamba kuna pesa ambazo huwa zinatolewa kutoka kitengo cha usalama cha ujasusi kisha kutumiwa kuwahonga viongozi ili waegemee mrengo wa serikali.

Bw Gachagua mnamo Alhamisi alizindua chama chake kipya cha Democracy for the Citizens Party (DCP) alichosema kitashirikiana na vyama vingine vya upinzani kumtimua Ruto mamlakani baada ya muhula huu wa kwanza.