Mkicheza mtafuata Gachagua nje, Ruto aonya ‘waenezao ukabila’ serikalini
RAIS William Ruto ameapa kumfuta kazi kiongozi yeyote ambaye ataendelea kueneza chuki, ukabila na migawanyiko miongoni mwa Wakenya, akiahidi kuendelea kuunganisha nchi.
Katika shambulizi la moja kwa moja dhidi ya aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, Dkt Ruto alisema tayari ametoa mfano kwa kuwatimua baadhi ya watu wanaoeneza migawanyiko na ukabila.
Mnamo Agosti 31 mwaka huu, Rais Ruto alikamilisha ziara yake ya siku nne Nyanza kwa mikutano ya hadhara katika eneo la Kondele la Kisumu ambako aliahidi kuunganisha nchi chini ya Serikali Jumuishi.
Ilikuwa siku chache tu baada ya kuwateua maafisa wanne wakuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kuwa mawaziri.
Jumanne, alikaribishwa kishujaa alipotembelea eneo hilo na kuchukua nafasi hiyo kumshambulia naibu wake aliyetimuliwa akidai alikuwa akieneza ukabila na ubaguzi miongoni mwa Wakenya.
‘Nitaunganisha nchi nzima’
“Nilisimama hapa Kondele na kusema kuwa nitaunganisha nchi nzima. Wale ambao wamekuwa wakieneza chuki, ukabila, migawanyiko na ubaguzi wameonyeshwa mlango. Tutaendelea kutimua wale wanaoendeleza maovu haya na kuwagawanya Wakenya,” akasema Dkt Ruto.
Pia alisema kwamba, alitekeleza jukumu muhimu kuhakikisha kuwa Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Muungano Mkuu baada ya kufanya kazi naye kama naibu kiongozi wa Chama cha ODM na akasema kuungana naye serikalini sio jambo gumu.
Alisisitiza kuwa viongozi hao wawili wakuu nchini wamekubaliana kukomesha siasa za ukabila, migawanyiko na utengano na badala yake wameungana kuwahudumia wananchi wa Kenya.
Huku akiomba wakazi kuunga mkono Serikali Jumuishi, Dkt Ruto alisema Bw Odinga alikuwa akirudisha mkono kwa kumsaidia kusimamia serikali.
“Nilikuwa hapa Kondele siku moja na nikawaambia kuwa niliwahi kumsaidia Agwambo (Raila). Wakati huu amenirudishia mkono na kunisaidia pia. Je, kuna tatizo na hilo?
Je, tuendelee kufanya kazi pamoja?” Dkt Ruto alisema, huku umati ukiitikia kwa kukubaliana naye.
Kiongozi wa nchi aliapa kuendelea kufanya kazi na viongozi na watu kutoka kila pembe ya nchi akisema hiyo ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo bila sehemu ya nchi kuhisi kutengwa. Alisema kuwa ataendelea kuiunganisha nchi chini ya Serikali Jumuishi ili kujenga taifa imara.
Kumuunga mkono Raila kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika
Rais pia alisisitiza kumuunga mkono Odinga katika azma yake ya kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.
“Niliahidi nitamshika Raila mkono na kuunga mkono azma yake.Hivi tunapozungumza, yuko nje ya nchi na amekuwa nchini Ivory Coast, Senegal na leo yuko Nigeria akitafuta kuwa Mwenyekiti wa AUC. Tuendelee kumuombea,” akasema.
Alipozuru Kisumu Agosti 31, aliandamana na Bw Gachagua na viongozi wengine lakini jana, naibu wake mpya Kithure Kindiki hakuwepo.
Dkt Ruto alikuwa na viongozi kutoka eneo hilo wakiwemo Magavana Anyang Nyong’o (Kisumu), James Orengo (Siaya), Gladys Wanga (Homa Bay) na wabunge Dkt Joshua Oron (Kisumu ya Kati), James K’oyoo (Muhoroni), Samuel Atandi. (Alego Usonga), Felix Jalang’o (Langata) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.
Rais alisema atarejesha mpango wa ‘Kazi Mtaani’ mjini Kisumu Januari mwaka ujao kufuatia ombi la Mbunge wa Kisumu ya Kati Dkt Joshua Oron.
Dkt Ruto alimhakikishia Gavana Nyong’o kwamba, miradi ya nyumba za bei nafuu, sekta ya sukari na uvuvi katika kaunti hiyo, itakamilika.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA