Shangazi Akujibu

Mama mkwe ananitongoza, nitamkomeshaje?

Na PAULINE ONGAJI November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Vipi shangazi?

Nina tatizo na mama mkwe wangu. Tangu nioane na bintiye, amekuwa akiniandama huku akitaka nilale naye. Hata hivi majuzi ameanza kunitumia jumbe za mapenzi kupitia simu. Nimkomesheje?

Salama!

Balaa hiyo! Huo ni mwiko mkubwa sana. Mkanye kikamilifu kabla ya kumwambia bintiye kwani akijua huenda uhusiano wao ukavunjika.

Ratiba yake ya mahaba yaniumiza sana!

Shikamoo shangazi?

Mke wangu wa miaka miwili ameanza tabia ya kuunda ratiba ya mahaba. Mwanzoni alikuwa amepanga tushiriki tendo la ndoa angaa mara moja kwa wiki. Sasa amepunguza na kuwa mara mbili tu kwa mwezi. Nimwambieje kwamba naumia?

Marahaba!

Zungumza naye kwani huenda kuna jambo linamtatiza. Aidha, ni wakati wa kumhusisha mshauri nasaha katika mjadala wenu ili muweze kupata suluhu ya kudumu.

Sina haja kabisa na wanaume wa Kiafrika

Mpendwa shangazi,

Katika maisha yangu ya uchumba nimekutana na wanaume wa Kiafrika ambao wamenisababishia majonzi na hasara kubwa. Sasa nataka kuolewa na kamwe simtaki mwanamume wa Kiafrika.

Bila shaka una uhuru na haki ya kumchagua umpendaye, lakini kutumia msingi wa rangi au asili si kigezo kizuri cha kumtafuta mume. Japo ikiwa kwa kweli unawataka wanaume wa asili nyingine, nenda kwenye mitandao ya kusaka wapenzi ujaribu bahati yako.

Rafiki yangu mjakazi anamtumbuiza tajiri wake Uarabuni

Hujambo shangazi?

Rafiki yangu alihamia Saudia miezi mitano iliyopita ambapo alienda kufanya kazi kama mjakazi.

Lakini sasa ananiambia kwamba amekuwa akishiriki mapenzi na mume wa tajiri wake kila mara, na hata jamaa huyo ameahidi kumnunulia nyumba. Nimshauri vipi?

Hiyo ni hatari kubwa sana hasa ikizingatiwa kwamba anaishi katika nchi ya kigeni; taifa ambalo limenakili visa vingi vya mabinti wetu kuuawa kwa njia tatanishi. Mke wa mwanamume huyo akigundua bila shaka mambo hayatamwendea vyema rafiki yako.​