Mkurugenzi wa mawasiliano katika afisi ya Mudavadi akamatwa kwa tuhuma za ulaghai
MKURUGENZI wa Kitengo cha Habari katika Afisi ya Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni, Musalia Mudavadi, Salim Swaleh Jumamosi, Juni 22, 2024 alikamatwa na maafisa wa upelelezi wa jinai kwa kushiriki ulaghai.
Mnamo Jumapili Juni 23, 2024, Afisi ya Mudavadi ilithibitisha kukamatwa kwa afisa huyo baada ya washukiwa wa ulaghai/utapeli kupatwa katika afisi yake iliyoko katika jengo la Shirika la Reli Nchini (KRC), Nairobi.
Walaghai hao walipatikana na kadi bandia za kufungua milango.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Masuala ya Mawasiliano katika Afisi ya Bw Mudavadi Peter Warutere alisema kuwa maafisa kadhaa wa serikali na walaghai walikamatwa pamoja na Swaleh.
“Genge la walaghai na maafisa wa serikali walioendesha maovu yao katika Afisi za Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni (OPCS-MFDA) katika jengo la Shirika la Reli Nchini walikamatwa jana, Jumamosi Juni 22. Miongoni mwao ni Mkuu wa Kitengo cha Habari katika afisi hii. Uchunguzi zaidi unaendeshwa kwa lengo la kuwanasa washirika wengine ambao huenda walihusika katika uovu huo,” Bw Warutere akasema katika taarifa hiyo.
Kukamatwa kwa watu hao kulifanyika baada ya walinzi wa Mudavadi kupashwa habari kuhusu vitendo vyao.
Bw Swaleh, ni mwanahabari mtajika, amewahi kuhudumu katika mashirika kadhaa ya habari nchini ikiwemo NTV kabla ya kuteuliwa kwa wadhifa huo mnamo Januari 2023.
Aidha, aliwahi kuhudumu, kwa muda mfupi, kama Afisa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano katika Kaunti ya Nakuru.