Mshiriki asimulia jinsi Mackenzie alichukua mifugo wake kama adhabu
MSHIRIKI katika kanisa la Good News International linalohusishwa na Paul Mackenzie amesimulia mahakama jinsi kiongozi huyo wa dhehebu na watu wake walivyochukua mifugo wake katika msitu wa Shakahola.
Shahidi huyo alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu, Leah Juma kwamba alipoteza kuku na sungura wake baada ya kuchukuliwa na wazee waliokuwa wakifanya kazi chini ya Mackenzie.
Kulingana na ushahidi wake, Mackenzie alikuwa ametoa maagizo ya kuzuia mtu yeyote kufuga wanyama wa kufugwa na ndege msituni.
“Nilikuwa nimefuga kuku na sungura kwa kutarajia kujiendeleza lakini walitoweka. Nilipoulizia, niliambiwa kwamba wazee walikuwa wametumwa nyumbani kwangu kuchukua mifugo wangu,” aliambia mahakama wakati akihojiwa na waendesha mashtaka Jami Yamina, Ogega Bosibori na Anthony Musyoka.
Shahidi huyo alisema baraza la mawaziri wa Mackenzie walihakikisha kwamba sheria zake zinafuatwa na kwamba aliyekosa kuyafuata angeadhibiwa.
Baraza hili la mawaziri lilisimamia miji kama Yudea, Bethlehemu, Galilaya na mingine mingi kadri maeneo yalivyopangwa.
Baraza la mawaziri pia lilihakikisha kuwa mikutano iliyofanywa na kuhutubiwa na Mackenzie ilitangazwa siku moja kabla ya kufanyika.
Shahidi huyo pia alisema kuwa Mackenzie si tu kwamba alipiga marufuku ufugaji bali pia aliwazuia wafuasi wake kuwaruhusu watoto wao kuenda shuleni na alipiga marufuku juhudi zozote za mtu kujiendeleza na kufanikiwa.
Mahakama pia ilielezwa kuwa Mackenzie na mkewe Rhoda Mumbua Maweu walimpigia simu shahidi huyo mara kadhaa wakimtaka ahamie msituni kuabudu pamoja nao na pia kununua shamba ndani ya msitu huo.
Shahidi huyo alisema alipuuza ombi la kujiunga na kanisa mara nyingi lakini alikubali shinikizo mnamo 2022 na kuhamia msituni.
“Nilikubali baadaye na kununua ekari mbili kutoka kwa Mackenzie kwa gharama ya Sh3,000 ambazo nililipa pesa taslimu,” alisema.
Lakini kutokana na changamoto za kifedha, shahidi huyo alisema hakuhamia katika ardhi hiyo mara moja.
“Kwa sababu ya kuchelewa kwangu, shamba langu liligawiwa mtu mwingine, lakini niliendelea kushinikizwa kupata sehemu tofauti na kuhamia huko,” alisema.
Ardhi ya ukubwa wa ekari mbili
Shahidi huyo alisema kwamba alilazimika kununua sehemu nyingine ya ardhi yenye ukubwa wa ekari mbili kwa gharama ya Sh6,000.
Baada ya kuhama na kutulia ndani ya msitu huo, shahidi huyo asema alianza kujionea tabia na sheria za maisha ya huko zisizo na mantiki.
Shahidi huyo alisema kwamba makazi ya Makenzie anayafahamu kwa kuwa amemtembelea karibu mara tatu wakati akimpelekea fedha na mara nyingine wakati wa kusafisha bwawa lake la kuhifadhia maji.
Mackenzie, mkewe na watu wengine 93 wamekana makosa manne yanayohusiana na ugaidi.
Mackenzie almaarufu Mtumishi, Nabii au Papaa, Bi Maweu, Smart Mwakalama na mkewe Mary Kadzo Kahindi na watu wengine 28 walishtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na uhalifu wa kupangwa na kusababisha vifo vya wafuasi 429 wa kanisa hilo.
Mackenzie, Bi Maweu, Bw Kwakalama, mkewe na wenzake 28 pia wanashtakiwa kwa itikadi kali.
Serikali ilidai kuwa washukiwa hao waliendeleza mfumo wa imani hatari kwa madhumuni ya kuwezesha vurugu za kiitikadi hadi kufa kwa waumini kupitia kwa mfungo.