Mshukiwa wa mauaji ya Mwingereza Campbell Scott kusalia gerezani
MSHUKIWA katika mauaji ya raia wa Uingereza Campbell Scott atasalia gerezani kwa muda wa siku 53, hadi ripoti kubaini ikiwa akili yake ni timamu kufunguliwa mashtaka ya mauaji itakapowasilishwa kortini.
Alex Mutua Kithuka alitarajiwa kusomewa shtaka la kuua Scott Feburuari 16, 2025 lakini akarudishwa gerezani.
Kithuka alifahamishwa na naibu wa msajili wa mahakama kuu Makadara kwamba ripoti ya utimamu wa akili yake haijawasilishwa wa kortini.
Pia, alielezwa wakili wa kumtetea hajateuliwa.
Kithuka alikuwa amezuiliwa pamoja na Albanus Mutinda Nzioka aliyeachiliwa huru baada ya DPP kusema hakuhusika na mauaji ya Scott.
Kithuka alifikishwa mbele ya Jaji James Wakiaga lakini hakutakiwa kujibu shtaka hadi pale ripoti ya utimamu wa akili yake itakapowasilishwa mahakamani.
Hali kadhalika, alielezwa Mwanasheria Mkuu bado hajamteua wakili wa kumtetea katika kesi hiyo.
Kithuka aliambiwa na Jaji Wakiaga kwamba Mwanasheria Mkuu anatakiwa kisheria kumteua wakili wa kumtetea kwa vile akipatikana na hatia adhabu atakayopata ni kifo.
Jaji Wakiaga alimweleza Kithuka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga aliamuru ashtakiwe kwa mauaji ya Campbell Scott Alistair katika mtaa wa Pipeline Nairobi mnamo Feburuari 16, 2025.
Maiti ya Scott iliokotwa ndani ya msitu wa Makongo, Kaunti ya Makueni.
Albanus Mutinda aliponyoka baada ya DPP Renson Ingonga kuamuru aachiliwe.
“Baada ya kutathmini ushahidi wote, nimefikia uamuzi Albanus Mutinda Kithuka hakuhusika katika mauaji ya Scott. Aachiliwe huru,” DPP alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina mnamo Machi 25, 2025.
Kithuka aliagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani ambapo alitolewa Machi 26, 2025 kushtakiwa kwa mauaji.
Uamuzi wa DPP kumshtaki Kithuka uliwasilishwa kortini na kiongozi wa mashtaka Joyce Olajo.
“Nimeagizwa nifahamishe hii mahakama kwamba Kithuka atashtakiwa kwa mauaji ilhali Albanus aachiliwe huru,” Bi Olajo alidokeza.
Alex na Albanus walikamatwa Machi 1, 2025 katika barabara ya Nairobi-Mombasa, hakimu alifahamishwa.
Mauaji ya Scott yalizua hisia kali huku uhusiano wa Kenya na Uingereza ukiigia mchanga lakini polisi walifanya juu chini kuhakikisha waliohusika wamekamatwa na kushtakiwa.
Mmoja wa washukiwa waliodhaniwa kuhusika alijiua mtaani Dandora Nairobi.
Mahakama ilielezwa kuwa kadi za benki za marehemu zilijaribiwa kutoa pesa mjini Voi, Mombasa na NairobI.
Sasa Kithuka amezuiliwa katika gereza la Viwandani akisubiri kuwasilishwa kwa ripoti ya ikiwa akili yake ni timamu kusomewa shtaka la mauaji.
Kithuka atarudishwa kortini baada ya Mahakama Kuu kukamilisha likizo yake ya Pasaka itakayoanza Aprili 9, 2025.