Mtetezi wa haki Khelef Khalifa achunguzwa kwa uchochezi
MTETEZI wa haki za binadamu, Bw Khelef Khalifa, sasa yumo hatarini kushtakiwa kwa madai ya kueneza uchochezi wa kidini na kijamii katika Kaunti ya Lamu.
Hii ni baada ya Tume ya Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kumwagiza kufika mbele ya tume ili ahojiwe, kama sehemu ya uchunguzi wa matamshi aliyotoa wikendi yaliyoibua hisia kali.
Mwenyekiti wa NCIC, Dkt Samuel Kobia, alisema kwenye taarifa kwamba matamshi ya Bw Khalifa ni sawa na kualika vita, hali ambayo haistahili kamwe nchini.
“Kulingana na Katiba, Wakenya wana uhuru wa kuishi, kufanya biashara, na kushiriki katika masuala ya kaunti na kitaifa mahali popote nchini,” akasema.
Dkt Kobia aliongeza kuwa, tume hiyo itaandaa mikutano na viongozi wa kisiasa, kidini, vijana na kijamii katika Kaunti ya Lamu ili kujadiliana kuhusu jinsi ya kuendeleza umoja katika jamii.
Bw Khalifa, mkurugenzi wa shirika la Muslims for Human Rights (MUHURI), aligusia masuala nyeti kama vile umiliki wa ardhi, kutengwa kwa masuala ya usalama na maendeleo, ukosefu wa haki katika utawala na uwakilishi wa kisiasa wa wale aliowataja kuwa watu asili wa Lamu katika hotuba ambayo imeibua hisia kali hasa eneo la Pwani.
Alipohojiwa na Taifa Leo awali, Bw Khalifa alisisitiza kwamba hataomba msamaha kwa kusema ukweli.
“Sijutii nilichosema. Nikipewa jukwaa, nitalisema tena na tena hadi serikali isikie na kuhutubia,” akasema Bw Khalifa.
Awali, Seneta wa Lamu, Bw Joseph Githuku Kamau, aliiandikia barua NCIC akitaka kikundi cha ‘Wanati wa Lamu’ kichunguzwe kwa madai ya uchochezi.
Katika barua hiyo iliyotumwa kwa Dkt Kobia, seneta huyo alieleza wasiwasi wake kutokana na matamshi ya hivi majuzi ya wanachama wa kundi hilo.
Bw Githuku aliithibitishia Taifa Leo kwamba malalamishi yake yanatokana na tukio lile lile ambapo mwanaharakati wa haki za binadamu, Bw Khelef Khalifa, alinaswa kwenye video akitoa matamshi yanayoaminika kuwa ya uchochezi.
Kulingana na seneta huyo, kundi la Wanati wa Lamu, linalodaiwa kuwa na Masheikh na wafanyabiashara mashuhuri, mnamo Novemba 22, 2024, walikutana katika baraza la umma ambapo walitoa matamshi ambayo yanachochea migawanyiko na chuki.
Aidha aliongeza kuwa matamshi kama hayo yanaweza kuathiri utangamano uliodumu kwa muda mrefu miongoni mwa jamii mbalimbali za Lamu, ambazo zimeishi pamoja kwa amani bila kurejelea misimamo ya kidini au kikabila.
Seneta huyo alilalamika kwamba, matamshi yanayotolewa na ‘Wanati wa Lamu’ sio tu ya kuleta migawanyiko bali pia ni matamshi ya chuki, jinsi inavyofafanuliwa chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, na kutishia kupanda mbegu za migawanyiko ya kikabila na kidini.
Bw Githuku alisema, “Hii ni njia hatari ambayo inaweza kusababisha ukosefu wa utulivu Lamu na maeneo mengine ya nchi.”
Seneta huyo aidha anataka kundi hilo liwajibike na iwapo hatua zao zitabainika kukiuka sheria, tume hiyo ichukue hatua ifaayo kuzuia kuenea zaidi kwa itikadi hizo zinazozusha mgawanyiko.
Zaidi ya hayo, aliomba NCIC kuendeleza juhudi za upatanisho katika Kaunti ya Lamu kwa kufanya kazi na wadau wa eneo hilo ili kuimarisha maadili ya utangamano, kuheshimiana na kuishi pamoja kwa amani.
“Mheshimiwa mwenyekiti, kama taasisi iliyopewa mamlaka ya kukuza umoja wa kitaifa, hatua yako ya haraka kuhusu suala hili itatuma ujumbe mzito kwamba Kenya haitavumilia aina yoyote ya matamshi ya migawanyiko au ubaguzi kwa misingi ya ukanda, kabila, au misimamo ya kisiasa,” akasema Bw Githuku katika barua hiyo ya Jumanne, Novemba 26.
Hata hivyo, kiongozi wa Kundi la Wanati, Bw Sultan Omar Shariff alipuuzilia mbali madai ya seneta huyo ya uchochezi na kundi hilo.
Bw Omar alisisitiza kuwa, wanachoshinikiza ni haki kwa wenyeji wa Lamu na si chochote kingine.
“Seneta anafaa kukoma kuhangaika na kukwepa ukweli uliopo. Kuna dhuluma nyingi za kihistoria zilizofanywa kwa watu wa Lamu zikiwemo umiliki wa ardhi, uwakilishi wa kisiasa, maendeleo na kubaguliwa kabisa,” akasema Bw Shariff.