Mtihani kwa Sakaja uchafu Nairobi ukimuudhi Ruto
RAIS William Ruto ameonekana kulenga utawala wa Gavana Johson Sakaja, akisema kuwa uchafu ambao umekuwa ukishihudiwa jijini Nairobi ni wa kuabisha nchi.
Akiongea Jumatatu katika Mkutano na Maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO), Rais alisema juhudi zinahitajika kuhakikisha jiji la Nairobi ni safi na pia mto Nairobi unasafishwa na kurejeshewa hadhi yake.
“Nairobi ni jiji letu na ndiyo sura ya Kenya na inafanya wale ambao wanatutembelea wawe na dhana kuhusu taifa letu. Hatuwezi kuendelea hivi na tuambiane ukweli,” akasema Rais
“Ukipita kila mahali unapata uchafu, mabomba ya maji taka, mifuko ya plastiki na sasa hata viwanda vinaachia uchafu na kuuelekeza jijini,” akaongeza.
Utawala wa Gavana Sakaja umekuwa ukikashifiwa kwa kuwa na mpangilio mbaya wa jiji huku wachuuzi wakiwa wamejaa kila mahali na kufika hata katikati mwa jiji.
Rais alisema kuwa Nairobi ndiyo makao makuu ya Shirika la Umoja wa Kimataifa Kuhusu Mazingira na lazima iwe safi badala ya kuelekea majitaka kutoka mto Nairobi.
“Makao makuu ya shirika la mazingira halifai kuwa na uchafu na uvundo ambao unatoka mto Nairobi. Sote tushirikiane kuhakikisha kuwa tunatunza mto, jiji na mazingira ila kuafiki hadhi ya kuwa kitovu cha mazingira,” akaongeza Rais.
Alikuwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki na Bw Sakaja kati ya viongozi wengine.
Rais amekuwa akiongoza juhudi za kusafisha mto Nairobi ambao umekuwa kikwazo kwa tawala zilizopita. Kwa upande mwingine Bw Gachagua na Gavana Sakaja wamekuwa wakilumbana kuhusu kuhamishwa kwa wachuuzi katikati mwa jiji, suala ambalo sasa limechukua mkondo wa kisiasa.