Habari za Kitaifa

Mudavadi motoni kwa matamshi ya kumpendelea Raila

Na RUTH MBULA August 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi huenda akajipata motoni kufuatia matamshi ya hivi majuzi yaliyompendelea Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Hii ni baada ya Bw Mudavadi kusema kuwa Bw Odinga ndiye Mkenya pekee aliyeidhinishwa na serikali kuwania kiti hicho.

Hii ilikuwa licha ya Wakenya wengine kama vile Bw Jephnei Nyakwama Orina, 31, kuwasilisha ombi lake kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni mnamo Julai 22, 2024 bila kupewa majibu.

Bw Orina sasa ameagiza wakili wake Enock Ong’iti kumshurutisha Bw Mudavadi aombe msamaha na pia ajiuzulu kutoka ofisi ya umma.

“Katika kikao cha pamoja na wanahabari na Bw Raila Odinga… ulipuuza wagombeaji wengine na kuwataja kama ‘wasio muhimu’ na ukasisitiza kuwa serikali ina haki ya kuteua mgombeaji. Jibu lako linakiuka kanuni kadhaa za kikatiba,” alisema Bw Orina.

Malalamishi yake yalikuwa kwenye barua aliyowasilisha kwa afisi ya Bw Mudavadi mnamo Ijumaa.

Alisisitiza kuwa ukuruba wa serikali na kiongozi wa upinzani haufai kuwa sababu ya kuzuia Wakenya wengine waliohitimu kuteuliwa na serikali kuwania wadhifa kama huo.

“Licha ya uhusiano wako wa kisiasa na Bw Odinga, afisi yako ni ya umma inayofadhiliwa na walipaji ushuru na hivyo una jukumu la kutumikia Wakenya wote bila kujali maoni yao, kabila, wala misimamo yao ya kijamii na kisiasa kama inavyoamriwa katika Vifungu vya 10 na 27 vya Katiba ya Kenya,” barua hiyo ilieleza.

Kwa hivyo, Bw Orina anasema, haki yake ya kibinadamu na usawa ilipuuzwa kinyume na Kifungu 3 cha Katiba kinachomlazimu Bw Mudavadi kuheshimu, kudumisha na kutetea katiba.

“Kwa kutofahamisha taifa kwamba Wakenya wengine walituma maombi kuwania nafasi ya uenyekiti wa AUC, ulikiuka katiba na haki ya mteja wetu,” barua ya wakili ilihoji.Bw Orina anadai kuwa azimio la serikali la kumteua Bw Odinga bila kwanza kumhusisha katika mchakato wa ushindani baina yake na Wakenya wengine waliosaka kiti hicho cha AUC, sio haki wala utaratibu sawa.

Barua hiyo inasisitiza kwamba matamshi ya Mkuu wa Mawaziri yameondoa imani ya umma kwake, hivyo basi anapaswa kujiuzulu.

Inahitimisha kwa kusema kuwa nafasi ya mwenyekiti wa AUC inafaa kuwa wazi kwa Wakenya wote waliohitimu, na sio tu kwa tabaka la kisiasa.