Mudavadi: Mswada wa Fedha haufai kuangushwa, sababu hiyo ni sawa na kuangusha serikali
KINARA wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesema Mswada wa Fedha 2024 lazima upitishwe na kutiwa saini na Rais William Ruto kuwa sheria, akisema kinyume na hivyo itakuwa ni sawa na kuangusha Serikali.
Akizungumza mjini Kabarnet, Baringo ya Kati, Ijumaa, wakati wa hafla ya kuchangisha pesa kusaidia vikundi vya kina mama, Bw Mudavadi alisema serikali haiwezi kuendeshwa bila ushuru na madeni.
“Mswada wa Fedha lazima upite kwa sababu ukiangushwa ni sawa na kuangusha serikali. Kwa hivyo haya maandamano hayafai kupuuzwa kwa sababu wanachosema wanamaanisha wanataka kuangusha serikali,” akasema.
Mnamo Alhamisi Juni 20, 2024, Wabunge 204 walipiga kura kuvukisha mswada huo ambao unapingwa vikali na idadi kubwa ya wananchi haswa vijana, katika hatua iliyomaanisha kwamba unaingia katika “Committee Stage” ambapo mapendekezo ya kuondoa baadhi ya ushuru yatapigiwa kura.
Waandamanaji, wengi wao wakiwa chipukizi wa Gen Z wanataka mswada huo uangushwe, wala sio kukarabatiwa, wakisema kwamba licha ya mapendekezo ya kuondoa baadhi ya ushuru, bado kuna ushuru kwenye vipengele vingine ambao utafanya maisha kuwa magumu kuliko yalivyo sasa.