Habari za Kitaifa

Murkomen amtetea Kahariri kuhusu msimamo wa jeshi wa kauli ya “Ruto Must Go”

Na CHARLES WASONGA March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewatetea wakuu wawili wa vitengo vya usalama waliowakashifu wale wanaoendeleza kampeni za kushinikiza Rais William Ruto aondoke mamlakani.

Bw Murkomen Jumapili, Machi 30, 2025, alisema Mkuu wa Majeshi Charles Kahariri na Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Noordin Haji walipinga kampeni za “Ruto Must Go” (Sharti Ruto Aondoke) kwa ufahamu kuwa zinaweza kuleta machafuko nchini.

“Jenerali Kahariri na Mkuu wa NIS Haji walitoa kauli hiyo kwa sababu wana habari kwamba kauli kama hizo zinaweza kuleta mchafuko nchini. Kwa hivyo, wale wanaowashutumu wajue kwamba uthabiti wa taifa hili una umuhimu mkubwa zaidi,” Waziri huyo akasema alipohutubia waumini katika Kanisa la AIC Makutano, eneobunge la Imenti Kaskazini, Meru.

Jenerali Kahariri na Bw Haji walitoa kauli hiyo Alhamisi, Machi 27, 2025 wakati wa mhadhara wa umma katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Ujasusi na Utafiti (NIRU), mtaani Karen, Nairobi.

“Hata huku wananchi wakifurahia uhuru wao wa kujieleza, sharti kuwe na mipaka katika kufanya hivyo. Hizo kauli za ‘Must Go’ sharti zitolewe kulingana na Katiba,” Jenerali Kahariri akaeleza.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) halijihusishi na siasa na wajibu wao wa kipekee na kulinda nchi huku likiunga serikali iliyoko mamlakani kwa misingi ya kikatiba.

Lakini baada ya kauli hiyo ya Jenerali Kahariri, Wakenya na viongozi wa kisiasa walidai kuwa anavuka mipaka kwa kuingililia siasa.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Chama cha Peoples’ Liberation Party Martha Karua na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa ni miongoni mwa viongozi waliowashutumu Jeneral Kahariri na Bw Haji.

“Koma kuingilia siasa kwa sababu wewe ni mwanajeshi. Hata kama unataka kumtetea Rais Ruto fanya hivyo ndani ya kambi ya jeshi usije ukaleta shida nchini Kenya,” Bw Gachagua alimwambia Jenerali Kahariri Jumamosi akiwa mjini Naivasha.