Habari za Kitaifa

Mwalimu wa kiume aliyejifanya bintiye rais Ruto asukumwa korokoroni

Na RICHARD MUNGUTI April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWALIMU mwanaume anayedaiwa akujifanya bintiye Rais William Ruto, June Ruto, amefikishwa kortini.

Samuel Mogwasu Mainga, kutoka Kaunti ya Nyamira alifikishwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi Alhamisi (Aprili 10, 205) alasiri.

Mainga aliyetiwa nguvuni mjini Mombasa Aprili 9,2025 aliagizwa na hakimu mwandamizi Robinson Ondieki azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Aprili 11, 2025 atakapoamua ikiwa atamwachilia kwa dhamana.

Mainga, mahakama ilielezwa na afisa wa polisi Konstebo Peter Mwangi kwamba, mwalimu huyo alijifanya bintiye Ruto katika jumbe alizotuma katika mtandao wake wa Facebook kati ya Machi 30 na Aprili 8, 2025.

“Naomba mshukiwa huyu (Mainga) azuiliwe kwa siku saba nikamilishe uchunguzi na kuandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi,” Konstebo Mwangi alimweleza hakimu.

Pia, hakimu alielezwa kwamba polisi wanataka kubaini ikiwa mshukiwa amepeperusha jumbe akijatambulisha kuwa yeye ni June Ruto.

Wakili Danstan Omari anayemwakilisha mshukiwa huyo aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana.

“Mwalimu huyu wa Sekondari ya Msingi (JSS) alitiwa nguvuni na polisi akiwa anahudhuria hafla za michezo mjini Mombasa alipokuwa amepeleka wanafunzi kutoka Nyamira,” Bw Omari alidokeza.

Wakili huyo alisema baada ya kutiwa mbaroni na kusafirishwa hadi Nairobi, Mainga aliwaacha wanafunzi peke yao na “hajui hali yao sasa.”

Bw Omari aliomba mahakama imwachilie Mainga kwa dhamana akisema polisi wanaweza kuchunguza kesi hiyo mshukiwa akiwa nje.

Pia, alisema mahakama inaweza amuru Mainga awe akipiga ripoti kwa polisi kabla ya uchunguzi kukamilishwa.