Habari za Kitaifa

Mwanamke aliyepata mimba akiwa kwenye ibada za Shakahola atibiwa maradhi ya akili

January 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

Mama aliyeokolewa katika msitu wa Shakahola amelazwa katika hospitali ya Port Reiz mjini Mombasa kwa matibabu ya kiakili huku serikali ikitafakari hatua zaidi itakayomfaa.

Mwanamke huyo, FM, ni mmoja wa watu 66 waliookolewa kutoka msituni Mei 2023, ambapo mhubiri tata Paul Mackenzie na mamia ya wafuasi wake walikuwa wamekusanyika kufunga hadi kufa.

Soma Wafukuaji wa maiti Shakahola wafunguka

Kwa sasa, serikali imesema kuwa haitamchukulia kama mshukiwa, kwani ripoti za awali za matibabu zilionyesha kuwa hayuko sawa kiakili kushtakiwa.

Upande wa mashtaka umetupilia mbali mashtaka yote dhidi yake ambayo yalipaswa kupendekezwa dhidi yake na washirika wake kwa sasa, na kupendekeza apelekwe hospitali kuchunguzwa hali yake ya kiakili.

“Hatumchukulii kama mshukiwa tena. Tunapendekeza afanyiwe uchunguzi upya ya akili kabla hatujachukua hatua nyingine kama vile kumwachilia aende kwa familia yake,” alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma Jami Yamina.

Bw Yamina alisema kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa mwanamke huyo atakuwa sawa kabla ya kuchukua hatua zozote, ikiwa ni pamoja na kumchukulia kama shahidi wa serikali.

“Mwanamke huyo ana mtoto wa miezi miwili ambaye alizaliwa akiwa kizuizini,” mwendesha mashtaka alisema.

Mwanamke huyo aliwashangaza watu mahakamani alipojitokeza akiwa na mtoto mchanga.

Soma Shakahola: Mshangao kubainika mshukiwa alijifungulia gerezani

Mama huyo alipewa ulinzi mkali na askari wa gereza katika eneo la mahabusu ndani ya mahakama kabla ya kufikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkuu Joe Omido pamoja na washirika wake.

Mwanamke huyo ni miongoni mwa watu 66 ambao awali walizuiliwa katika Kituo cha Uokoaji cha Sajahanad huko Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, baada ya kuokolewa kama manusura wa mauaji ya Shakahola.

Soma Shakahola: Waliookolewa wageuzwa kuwa mashahidi

Mahakama ilisikia kuwa mtoto huyo mchanga alizaliwa miezi miwili mapema katika gereza la Shimo La Tewa.

Hii inamanisha kuwa huenda mwanamke huyo alishika ujauzito akiwa katika msitu wa Shakahola na kujifungua akiwa kizuizini.

Muda huu unaonyesha kwamba mwanamke huyo alipata mimba msituni kabla tu ya mkasa huo kuibuliwa.

Mahakama haijaambiwa kama mwanamke huyo alikuwa na mumwewe kwenye msitu huo.