Habari za Kitaifa

Mwanamke mjini Kisumu akamatwa kwa kurekodi video chafu na mwanawe ili kuuza mtandaoni

Na RUSHDIE OUDIA March 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMKE mmoja mjini Kisumu, amekamatwa kwa madai ya kunyanyasa mtoto kingono baada ya video kusambazwa mtandaoni akidaiwa kushiriki tendo la ndoa na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 14.

Kulingana na polisi, mwanamke huyo anashukiwa kumhusisha mtoto wake wa kiume wa gredi ya nane katika vitendo vya ngono lakini alitoroka mtego aliowekewa na majirani zake, ambao waliibua wasiwasi baada ya kutazama video hiyo mtandaoni.

Majirani hao walikuwa wamedai kuwa mwanamke huyo alikuwa akiuza video hizo kwa tovuti za ponografia za watoto. Tumeficha jina la mshukiwa ili kumlinda mtoto.

Video hiyo ilisambazwa mtandaoni na kuvutia wakazi wengi wa Kisumu.

Bw Stanley Koech, Naibu Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kisumu ya Kati, alisema walifahamishwa kitendo hicho saa moja usiku Alhamisi Machi 6 walipopokea taarifa kuhusu madai ya kunyanyaswa kwa mtoto.

Kulingana naye, ni video hiyo ambayo iliwafanya wachukue hatua.

“Polisi walichukua hatua mara moja na kumuokoa mtoto huyo, mvulana wa miaka 14 ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi. Mshukiwa aliyedaiwa kuhusika na ponografia ili kujinufaisha kifedha alikamatwa na anashughulikiwa kabla ya kufikishwa kortini haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Koech.

Kufikia Alhamisi jioni, habari zilikuwa zimesambaa na watumiaji wa mtandaoni walikuwa wakitolea habari kuhusu mwanamke huyo ambaye alikuwa amejificha.

Hata hivyo, alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Kondele Alhamisi jioni baada ya kupata habari alikuwa akisakwa  na polisi na umma.

Awali polisi walikuwa wameanza msako wa kumtafuta mshukiwa huyo kwa kuwahusisha walimu kutoka shule anakosoma mvulana huyo. Naibu mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa walimpeleka mtoto huyo polisi.

Baadaye alizuiliwa kwa muda mfupi katika kituo cha uokoaji ndani ya Kituo cha Polisi cha Kondele kabla ya kupelekwa katika makao ya  Watoto ya Agape kutunzwa na kupatiwa ushauri.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai walimsaka mshukiwa huyo kwa kutumia nambari yake ya simu, iliyokuwa karibu na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga saa 8.30 Alhamisi usiku.

Kufikia wakati huo, shinikizo kutoka kwa wakazi zilikuwa zikiongezeka na hii ilimfanya mwanamke huyo kujisalimisha kwa usalama wake.