Habari za Kitaifa

Mwanamume aliyefariki seli alipigwa kichwani – Ripoti

January 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UCHUNGUZI wa mwili wa mwanaume aliyefariki kwa njia ya kutatanisha baada ya siku nne katika seli za kituo cha polisi umebainisha kuwa alifariki kutokana na jeraha la kichwa.

Bw Festus Muthui, 26, alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Bondeni, Kaunti ya Nakuru, kwa siku kadhaa bila kufunguliwa mashtaka rasmi.

Mwanapatholojia wa serikali, Dkt Titus Ngulungu, aliyefanya uchunguzi huo katika mochari ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru, alibainisha kuwa chanzo cha kifo hicho ni jeraha la kichwa lililosababishwa na kifaa butu.

“Kwa mujibu wa uchunguzi wangu, natoa maoni kwamba chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kichwani lililosababisha kuumia kwa ubongo kwa jumla na damu kuganda chini ya ngozi ya ubongo kutokana na nguvu nyingi za majeraha ya kichwa,” alisema Dkt Ngulungu.

Uchunguzi huo ulifanyika mbele ya familia ya marehemu, maafisa wa Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA), na watetezi wa haki za binadamu.

Fundi huyo wa magari, alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Bondeni Desemba 20, 2024 baada ya mke wake wa zamani kumripoti kwa madai ya kutelekeza majukumu ya binti yao wa miaka 12.

Katika mahojiano ya awali, babake marehemu, Bw George Mutinda, alisema alipokea simu kutoka kwa mwajiri wa mwanawe Desemba 20, akimfahamisha kuwa mwanawe alikamatwa na alihitajika kusafiri hadi Nakuru.

Alipofika, alikutana na mkaza mwana, Bi Eunice Kimani, aliyedai Sh30,000 za malipo ya matunzo ya mtoto ambayo Bw Muthui hakuwa ametoa kwa muda.

Kwa mujibu wake, idara ya watoto ilimwagiza mwanawe kulipa Sh2,000 kila mwezi , lakini alikosa kulipa kwa wakati fulani, jambo lililomlazimu kuingilia kati na kulipa Sh5,400 na kuahidi kuongeza Sh15,000 baadaye.

Bw Mutinda alikubaliana na mkaza mwana kukutana kituoni siku ifuatayo, ili Bw Muthui aachiliwe huru.

Hata hivyo, alikuta mwanawe akiwa katika hali mbaya.

“Polisi aliyeitwa Bi Ann Achieng’ alituhudumia. Tulipomuomba kumwachilia mwanangu, alisema lazima azungumze na OCS Meshak Mwangangi. Baada ya dakika chache alirudi na kusema OCS alitaka Sh20,000,” alisema.

Aliongeza kuwa alitoka kwenda kutafuta pesa hizo, ambazo alielezwa kuwa ni dhamana ya pesa taslimu, na mwanawe aliachiliwa kutoka seli.

Cha kustaajabisha aligundua kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa imedhoofika sana, hivyo kumlazimu kumkimbiza hospitalini.

“Mtoto wangu alitibiwa na ripoti ya daktari ilionyesha alikuwa na msongo wa mawazo na akapewa dawa, lakini muda mfupi baada ya kutibiwa, OCS wa Bondeni aliniita tena na kutuma gari la polisi aina ya Landcruiser kumrudisha mwanangu kituoni ambapo alimkamata tena,” alisema.

Bw Mutinda anabainisha kuwa siku iliyofuatia alipigiwa simu na polisi, ambao walimhitaji haraka kituoni. Lakini alipofika, alishtuka kumuona mwanawe akiwa amelala chini kwenye seli bila fahamu.

“Nilimkimbiza tena hospitalini nikiwa na polisi watatu, ambapo muda mfupi baadaye ilitangazwa kuwa amefariki dunia,” alisema.

Mkurugenzi wa shirika la Nakuru Human Rights Network (NAHURINET), Bw David Kuria, alitoa wito kwa IPOA kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ili familia ipate haki.

“Kituo hiki sasa kinajulikana sana, kuna kisa kingine ambapo afisa mmoja alimpiga risasi msichana wa shule na hakijawahi kuchunguzwa. IPOA inafaa kushughulikia kesi ipasavyo,” alisema.