Habari za Kitaifa

Mwandani wa Ruto, Felix Koskei kutwaa nguvu za kuajiri

Na MOSES NYAMORI March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MZOZO unatokota kuhusu mswada mpya unaopendekeza Mkuu wa Utumishi wa Umma atwikwe mamlaka ya kuajiri watumishi wa umma, huku Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) katika ripoti yake ya ndani ikidai kuwa kuna njama ya kudhoofisha mashirika huru.

Ripoti hiyo kuhusu athari za mswada huo – baada ya Baraza la Mawaziri kuupitisha Machi 11, 2025 – imeutaja kuwa kinyume cha Katiba na jaribio la kutwaa mamlaka yake kwa mlango wa nyuma.

Ripoti hiyo, ambayo Taifa Leo imeipata kwa njia ya kipekee, iliandaliwa na timu ya wanasheria wa tume hiyo na kuwasilishwa katika kikao cha bodi yake.

Inaonya kuwa mswada huo pia unaingilia mamlaka ya bodi za utumishi wa umma za kaunti, Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC), Tume ya Huduma za Bunge (PSC), Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) pamoja na tume huru na ofisi huru za kikatiba.

Mswada huo, uliopendekezwa na aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, unapendekeza kuundwa kwa Kamati Kuu ya Uajiri na Uhamisho wa Watumishi wa Umma, ambayo itakuwa na mamlaka ya kuajiri na kuhamisha maafisa wa ngazi za juu katika utumishi wa umma – jukumu ambalo kwa sasa linatekelezwa na PSC.

Kamati hiyo itaongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma – kwa sasa Felix Koskei – na itajumuisha makatibu wa wizara za Utumishi wa Umma, Usalama wa Ndani, Kazi, Masuala ya Nje, Hazina ya Kitaifa, pamoja na afisa mkuu mtendaji wa PSC.

“Kamati itakuwa na jukumu la kuhamisha maafisa wa utumishi wa umma kulingana na vyeo vyao. Wizara inayosimamia masuala ya utumishi wa umma itatoa huduma za ukatibu kwa kamati hiyo,” inasema sehemu ya mswada huo.

Katika muhtasari wake, mswada huo unasema kuwa lengo lake kuu ni “kutoa mfumo wa jumla wa usimamizi bora wa wafanyakazi katika utumishi wa umma katika viwango vya serikali ya kitaifa na kaunti.”

“Mswada unalenga kuboresha taaluma, na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa kuweka majukumu, wajibu na kazi za ofisi mbalimbali na kamati zinazohusika na usimamizi wa wafanyakazi,” inaeleza sehemu ya mswada huo.

Mswada huo pia unapendekeza kuanzishwa kwa Kamati ya Ushauri wa Usimamizi wa wafanyakazi, Kamati ya Maendeleo ya Wafanyakazi, na Kamati ya Usimamizi wa Utendaji wa Wafanyakazi.

Kamati ya Ushauri wa Usimamizi wa Wafanyakazi itakuwa na jukumu la kutoa mapendekezo kuhusu ajira, uteuzi, kupandishwa vyeo, na uhamisho wa maafisa.

Katika ripoti yake, PSC chini ya uenyekiti wa Balozi Anthony Muchiri, imeeleza kuwa mswada huo unalenga kuondoa mamlaka yake kikatiba.

Tume hiyo inasema kuwa endapo mswada utaidhinishwa, utahakikisha kuwa majukumu yake makuu yanahamishiwa Wizara ya Utumishi wa Umma na kamati mbalimbali zinazopendekezwa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kazi pekee ya tume ambayo mswada haujaingilia ni ile ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazotokana na masuala ya ajira katika utumishi wa umma wa kaunti.

“Kutokana na uchambuzi wa mswada huu, lengo lake ni kunyakua mamlaka yote ya kikatiba ya tume, isipokuwa jukumu la kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu ajira katika kaunti,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa mswada huo ni jaribio la kufanya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuwa mwajiri mmoja, jambo ambalo linahujumu ugatuzi wa mamlaka.

“Katiba inatambua serikali ya kitaifa na kila serikali ya kaunti kama waajiri tofauti. Mswada huu unapendekeza kunyang’anya PSC pamoja na bodi za utumishi wa umma za kaunti mamlaka yao,” inasema ripoti hiyo.

PSC imehoji sababu ya mswada huu, ikieleza kuwa Katiba tayari inaeleza majukumu na mamlaka ya vyombo mbalimbali vya usimamizi wa wafanyakazi katika utumishi wa umma.

Kifungu cha 234 cha Katiba kinataja uteuzi wa maafisa wa utumishi wa umma kama sehemu ya majukumu ya PSC.

PSC pia inasema kuwa maendeleo ya wafanyakazi katika utumishi wa umma ni jukumu lake la kipekee ambalo limefafanuliwa wazi katika Sheria ya PSC na kanuni zake.

“Mapendekezo katika mswada huu ni ukiukaji wa Katiba na yanakinzana na Sheria ya PSC. Kwa mujibu wa maana ya ‘utumishi wa umma,’ mswada huu pia unaingilia mamlaka ya tume nyingine za huduma na bodi za utumishi wa umma za kaunti,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasisitiza kuwa tayari kuna Kamati ya Uajiri na Uhamisho wa Watumishi wa Umma ambayo imeanzishwa na PSC na inafanya kazi kwa niaba yake.

“Kuunda kamati nyingine isiyodhibitiwa na PSC kutaongeza mkanganyiko. Aidha, mswada huu unatoa nafasi kwa kamati hiyo kuhamisha wafanyakazi katika ngazi zote, jambo linalonyima mamlaka maafisa waliopo ambao si wanachama wa kamati hiyo,” ripoti inaongeza.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa kuna mswada mwingine wa Usimamizi wa Wafanyakazi wa Umma 2024 ambao tayari uko mbele ya Bunge la Taifa na haukiuki mamlaka ya mashirika huru.