Habari za Kitaifa

Mwangangi kuongoza bima tata ya SHA

Na FRIDA OKACHI April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziri Msaidizi wa Afya (CAS), Dkt Mercy Mwangangi amerejea serikalini, wakati huu akitarajiwa kupambana na changamoto zinazokumba utekelezaji wa Bima ya Afya ya Jamii (SHA) baada ya kuteuliwa kuongoza taasisi hiyo.

Waziri wa Afya Aden Duale, Ijumaa, Aprili 11, 2025 alimteua Bi Mwangangi kama Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA. Alipokezwa wadhifa huo baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwahoji na kuwapiga msasa watu 92 waliotuma maombi.

Watu 92 walituma maombi ya kupata kazi hiyo lakini wawili wakaorodheshwa na Bi Mwangangi akawapiku wenzake.

Kabla ya uteuzi huo, Dkt Mwangangi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Uimarishaji wa Mifumo ya Afya katika Shirika la AMREF Afrika.

“Wizara inampongeza Dkt Mwangangi kwa uteuzi wake na kumtakia kila la heri anapoanza kazi yake kama mkuu wa SHA. Tuna imani kwamba, ana uwezo kuiongoza SHA na kutekeleza majukumu ya taasisi hiyo,” akasema Bw Duale.

Dkt Mwangangi ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika sekta ya afya na ni kati ya waasisi wa Mpango wa Kutoa Huduma Sawa wa Afya kwa Wote (UHC).

Alihudumu CAS chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Rais wa sasa, Dkt William Ruto alikuwa naibu wa Bw Kenya – wadhifa aliohudumu mihula miwili (2013 – 2022).