Habari za Kitaifa

Mwenyekiti wa KNCHR Odede amefariki, tume yatangaza

Na BENSON MATHEKA, NDUBI MOTORI January 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ROSELINE Odhiambo Odede, Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), amefariki dunia, tume hiyo imetangaza.

Katika taarifa, Makamu Mwenyekiti wa KNCHR Raymond Nyeris Jumamosi alisema Odede alifariki Ijumaa baada ya kuugua kwa muda mfupi.

“Kifo chake cha ghafla ni pigo kubwa kwa Tume na Taifa kwa ujumla. Kama Tume tulipata fursa ya kuhudumu na Roseline Odede kama Mwenyekiti katika uongozi wa KNCHR,” Dkt Nyeris alisema.

Bi Odede, mtetezi mkuu wa haki za binadamu, aliteuliwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kuongoza shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu mwaka wa 2021.

Kabla ya uteuzi wake, alikuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya na aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya kupiga msasa majaji na mahakimu.

Kazi yake ya mwisho ilikuwa Desemba 26, 2024 alipotoa taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini.

Tume hiyo ilitoa takwimu zinazoonyesha kuwa watu 82 wameripotiwa kutekwa nyara katika muda wa miezi sita iliyopita, huku 29 wakiwa bado hawajulikani walipo.

“Kumekuwa na visa vingine 13 vya utekaji nyara au kutoweka kwa watu katika miezi mitatu ya hivi majuzi,”  ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Odede.

“Visa saba vya watu kutekwa nyara vya hivi majuzi viliripotiwa mwezi wa Disemba 2024, na sita kati yao bado hawajapatikana, na kufanya 29  idadi ya watu ambao bado hawajapatikana tangu Juni 2024.”

Kauli ya tume hiyo ilivuta hisia za jamii ya kimataifa iliyotaka kukomeshwa kwa utekaji nyara unaoendelea na kuheshimiwa kwa haki za binadamu na utawala wa Rais William Ruto.

Mnamo Juni 2024, wakati wa maandamano dhidi ya serikali, Bi Odede pia alitoa data inayoonyesha hali ya haki za binadamu nchini Kenya ilikuwa mbaya zaidi, huku waandamanaji waliokuwa wakidumisha amani wakishambuliwa, kujeruhiwa na kuuawa na polisi wenye silaha.

Rais Ruto katika mahojiano, alishutumu tume ya haki za binadamu kwa kubuni takwimu kuhusu waliouawa katika maandamano hayo.