Habari za Kitaifa

Mwili mwingine waopolewa kutoka Mto Yala

Na KASSIM ADINASI August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

POLISI mjini Siaya wameanzisha uchunguzi baada ya mwili wa mwanamme kuopolewa kutoka Mto Yala.

Mwili huo uligunduliwa na raia aliyekuwa akioga ufuoni.

Kulingana na mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu katika shirika la Haki Kwetu, mwili huo unafanana na wa raia wa asili ya Asia.

“Tulipata habari kuhusu mwili Ijumaa iliyopita. Raia aliyekuwa anaoga kando ya mto aliuona na akatufahamisha pamoja na polisi. Tulienda kwenye mto huo Jumanne ambapo polisi kwa usaidizi wa wapiga mbizi eneo hilo waliweza kuutoa mwili,” alisema Bw Otieno.

Tukio hilo la Jumanne liliibua kumbukumbu za wakati ambapo miili ilikuwa ikitolewa kwenye Mto Yala karibu kila siku miaka miwili iliyopita.

Kulingana na mwanaharakati, walipoupeleka mwili katika mochari ya Hospitali ya Yala, wasimamizi walikataa kuupokea, wakilalamika kuwa mto huo kwa mara nyingine unapata sifa mbaya kama eneo la kutupa miili.

“Swali ambalo tunajiuliza kama wakazi na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu ni mbona Mto Yala? Mbona iwe lazima miili kutupwa ndani ya mto na wanaohusika bado hawajulikani na wako huru?” Alihoji Bw Otieno.

Alisema waliupeleka mwili huo katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Siaya ambapo jamaa wa mhasiriwa waliutambua Alhamisi.

“Inashangaza kuwa usimamizi wa hospitali ya Yala, ambayo ni kituo cha umma, ulikataa mwili,” alisema.

Mwili umehifadhiwa mochari ukisubiri upasuaji huku uchunguzi ukiendelea.

Chifu wa Yala, Johannes Anam, alithibitisha tukio hilo akisema, “Polisi na DCI wanafuatilia suala hili.”

Si tukio geni

Miaka miwili iliyopita, Mto Yala uligonga vichwa vya habari baada ya miili 32 kuopolewa.

Baadhi ya miili ilikuwa imeanza kuoza, kulingana na mpasuaji wa serikali, Johansen Oduor.

Mpigambizi eneo hilo, Nicholas Okite, ambaye amehusika pakubwa na shughuli ya kutoa miili katika mto huo, alisema, katika mahojiano, kuwa baadhi ya miili ilikuwa imekatwakatwa na ilikuwa vigumu kuitambua.

“Idadi kubwa ya miili ilikwama kwenye Ndani Falls kwa sababu ya miamba ya mimea,” alifafanua.

Serikali iliahidi kuchunguza kuhusu vifo vya wahasiriwa wote na kuwakamata washukiwa kukabiliwa na sheria lakini hilo halikuwahi kufanyika.