Nani aliwaua vijana hawa? Kitendawili cha vijana watatu kuuawa Murang’a polisi wakikana kuhusika
VIJANA watatu waliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliojihami wakiwa na magari yasiyo na nambari za usajili katika kijiji cha Mutoho, Kaunti ya Murang’a, huku polisi wakikana kutekeleza mauaji hayo.
Mili ya watatu hao, ilichukuliwa na kupelekwa katika mochari na maafisa wa polisi Jumanne asubuhi, saa kadhaa baada ya kupigwa risasi.
Wakuu wa polisi katika kaunti walidai hawafahamu sababu ya mauaji hayo, licha ya ripoti kutoka kwa kamati ya usalama kuonyesha, washukiwa hao watatu, walihusika na uvamizi katika eneo hilo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Murang’a Kusini Bw John Kanda, alikanusha kufahamu ripoti ya washukiwa hao pamoja na operesheni ya polisi dhidi ya watatu hao.
“Ninachojua, tulifahamishwa na wanakijiji kuwa kuna mili mitatu isiyojulikana eneo la Mutoho. Tulichukua na kupeleka kwenye hifadhi ya maiti. Tukio hilo linachunguzwa,” alisema Bw Kanda.
Bw Martin Kamau aliyeshuhudia tukio hilo, alisema watatu hao waliuawa saa tatu usiku Jumatatu na watu walioonekana kuwa polisi.
“Watatu hao walikuwa kwenye gari moja. Gari lilisimama kwenye barabara ya Kenol-Murang’a. Waliposhuka kwenye gari hilo, magari mengine mawili yalisimama na kuanza kuwafyatulia risasi,” alisema Bw Kamau.
Aliongeza kuwa waliofyatulia watatu hao risasi wanaaminika kuwa polisi kutokana na ujasiri waliokuwa nao.
“Baada ya kuwaua, walichukua silaha ndogo kutoka kwa waathiriwa. Walivuta mili hiyo hadi kwenye kichaka kutoka kwa barabara na kuondoka kwenye eneo la tukio huku gari la watatu hao likiachwa,” aliongeza.
Bw Kanda alisema kuwa baadhi ya simulizi kutoka kwa mashahidi ni miongoni mwa mambo yanayochunguzwa.