NCIC yaripoti Gachagua bungeni kwa kupayuka
TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imeonya kuhusu kuongezeka kwa magenge ya uhalifu na taharuki ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Tume hiyo imeeleza kuwa ongezeko la hotuba za chuki na uchochezi wa kikabila, hasa kutoka kwa viongozi wa kisiasa, linaweza kuchochea ghasia kama zilizoshuhudiwa mara kadhaa katika uchaguzi.
Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, Mbunge wa Webuye Dan Wanyama na Mbunge wa Starehe Amos Mwago ni miongoni mwa waliotajwa na NCIC kuwa wanaoeneza hotuba za chuki za kikabila, hali inayochochea mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.
Ripoti ya tume hiyo, iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama, pia inahusisha ongezeko la makundi ya uhalifu na matamshi ya uchochezi wa kisiasa, hali inayozua hofu ya ghasia kabla ya uchaguzi.
Kamishna wa NCIC Philip Okundi alisema hali inazidi kuwa mbaya, huku magenge ya wahalifu yakianza kujipanga katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tunafanya kazi kwa ushirikiano na Wizara ya Masuala ya Ndani kwa sababu tumeona makundi ya uhalifu yakijitokeza. Tunahitaji kuchukua hatua kabla mambo hayajaharibika,” Bw Okundi alionya.
Kwa mujibu wa orodha iliyowasilishwa na NCIC mbele ya Kamati ya Bunge, Bw Gachagua, Wanyama na Mwago wote wanatuhumiwa kwa uchochezi wa kikabila.
Ingawa Bw Mwago tayari amefika mbele ya tume kwa mahojiano, Bw Gachagua na Wanyama bado hawajafanya hivyo.
Wengine waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Kamishna wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, anayeshutumiwa kwa kuajiri naibu chifu kwa njia ya magendo, mwanablogu Francis Gaitho anayeshtakiwa kwa matamshi ya chuki, na MCA wa wadi ya Kapkateny Joan Kirong.
Mapema mwezi huu, tume hiyo ilimuonya Gachagua dhidi ya kutoa matamshi yanayoweza kuchochea chuki za kikabila na vurugu nchini.
NCIC pia imeeleza changamoto zake za kifedha, ikionya kuwa ukosefu wa rasilimali unadhoofisha juhudi zake za kudhibiti hotuba ya chuki na kuzuia ghasia.
Wabunge walikubaliana na wasiwasi wa NCIC, huku Mbunge wa Homa Bay Town Opondo Kaluma akionya kuwa endapo hatua hazitachukuliwa, ghasia za 2027 zinaweza kuwa mbaya zaidi ya zile za 2007.
Wabunge hao walieleza hofu kwamba ‘ngoma za vita’ zinaendelea kupigwa kuelekea uchaguzi, wakionya kuwa kuibuka tena kwa magenge ya uhalifu ni jambo la kutia wasiwasi.
Hali hii inajiri wakati magenge hatari kama vile Jeshi la Mzee, Chinkororo, China Squad, Mungiki na American Marine, ambayo kihistoria yamehusishwa na ghasia za kisiasa, yakianza kuibuka tena nchini.