Ng’ang’ana kortini lakini ujue hata katika UDA tunakuvua mamlaka, Gachagua aambiwa
CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kimetangaza kwamba, hivi karibuni kitamteua Naibu Rais mteule Kithure Kindiki kama naibu kiongozi wa chama hicho mara tu kesi zinazoendelea mahakamani za kupinga kuondolewa kwa Rigathi Gachagua zitakamilika.
Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar jana alisema chama hicho hakitakubali Bw Gachagua kuendelea kuwa naibu kiongozi wa chama kutokana na kudorora kwa uhusiano wake na wabunge na chama hicho kwa kwenda kinyume na maadili yake na kudumaza ajenda yake ya maendeleo ya kitaifa.
“Hili ni suala la kisiasa tu. Hakuna mahakama inayoweza kukupa uongozi. Uhusiano tayari umedorora na hawezi kuendelea kuhudumu kama naibu kiongozi wa chama,” Bw Omar alisema jijini Nairobi.
“Tulikuwa tunasonga mbele kama chama na tulikuwa tumejitolea kuwaunganisha Wakenya bila kujali kabila zao lakini yeye (Bw Gachagua) anahubiri ukabila na ndiyo maana ilimbidi aende.
“Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya UDA, itatoa tangazo la kujaza nafasi ya Bw Gachagua chamani mara tu mahakama zitakapohitimisha kesi zinazoendelea, alisema.
“Tunaheshimu mahakama kama chama na tunachosubiri ni kukamilika kwa mchakato huu ili tuwe na kikao cha NEC kumpitisha Profesa Kithure Kindiki kuwa kiongozi wa chama,” alisema.
“Hili ni jambo ambalo litafanyika ndani ya dakika chache. Tukutane saa kumi na mbili asubuhi na ifikapo saa kumi na mbili na nusu tutakuwa tumemtangaza kuwa naibu kiongozi mpya wa chama.”
Viongozi hao wa UDA walisema kuwa bado hawatawaandama washirika wa Bw Gachagua lakini wakasisitiza kuwa, uamuzi wa kuwatimua kutoka kwa uongozi wa kamati za bunge utafanywa na wabunge.
“Hatuna kisasi kama chama. Wataendelea kuhudumu katika nyadhifa zao lakini kwa hakika kuna haja ya kujipanga,” Bw Omar aliongeza.