Ni zamu yetu kula: Ruto awarushia minofu Askofu Wanjiru, Omanga
RAIS William Ruto amemteua aliyekuwa Mbunge wa Starehe Margret Wanjiru kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Mito Nairobi, katika mabadiliko makubwa ambayo yamepelekea tume hiyo kuhamishwa kutoka ofisi ya rais hadi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji.
Uteuzi wa Askofu Wanjiru, unaonekana kama jaribio la Rais Ruto kufurahisha eneo la Mlima Kenya.
Haya yanajiri wakati uhusiano wa rais na eneo hili muhimu ambalo lilichangia pakubwa katika kuchaguliwa kwake ukisuasua kufuatia kutimuliwa kwa naibu wake Rigathi Gachagua.
Rais Ruto alimteua aliyekuwa seneta mteule Millicent Omanga katika tume hiyo mpya iliyoundwa ya wanachama 11, kupitia notisi ya gazeti la serikali Oktoba 25, 2024.
Bi Omanga katika siku za hivi majuzi amekuwa akizungumzia masuala ya utawala nchini.
“Mimi, William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, kwa kutumia mamlaka niliyopewa na Katiba na Sheria za Jamhuri ya Kenya, ninateua Tume ya Mito ya Nairobi,” ilisema notisi ya gazeti la serikali.
Katika uundaji upya wa tume hiyo, rais alibatilisha uteuzi wa mwenyekiti wa awali Dkt Pamela A. Olet.
Lakini amewabakisha Dkt Mumo Musuva na Grace Senewa Mesopirr na Eva Muhia.
Wanachama wengine wa Tume ya Mito Nairobi (NRC) ni pamoja na Bw John Kioli, Bw Amos Chege Mugo, Bi Carlotta Dalago, Bi Rael Chebichii, Bw Benjamin Langwen, na Bw Charles Karisa Dadu.