Nilifungiwa na maiti usiku, asema mwanamke aliyeshambuliwa mazishini
MWANAMKE aliyeshambuliwa wakati wa mazishi ya mume wake wa zamani Kaunti ya Nyamira ameongea kuhusu masaibu aliyopitia, ambayo pia yalimwacha na majeraha mabaya.
Mellen Mogaka alishambuliwa na kudhalilishwa baada ya kukataa kushiriki katika ibada ya mazishi—kutupa mchanga kwenye kaburi—wakati wa mazishi ya mume wake wa zamani, Joseph Osoro, mnamo Machi 21, 2025, katika eneo la Kiambere, Mwongorisi.
Mume wake wa zamani, ambaye alikuwa mwendesha bodaboda, alifariki katika ajali ya barabarani.
Akisimulia kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo, Mellen alieleza matukio yaliyopelekea kushambuliwa kwake.
Alifichua kuwa kabla ya kushambuliwa mnamo Machi 21, alikuwa amefungiwa ndani ya chumba pamoja na maiti ya mume wake wa zamani.
“Ninaishi Narok, lakini nilisafiri hadi Kaunti ya Nyamira kuhudhuria mazishi ya mume wangu wa zamani. Usiku wa kuamkia mazishi, nilifungiwa ndani ya chumba pamoja na jeneza la mume wangu wa zamani, ambako nililazimika kulala usiku mzima,” aliambia Taifa Leo.
“Siku iliyofuata, wakati wa ibada ya mwisho ulipofika, licha ya kupinga, wakwe zangu waliniburuta kwa nguvu, wakisisitiza kwamba ni lazima nishiriki katika ibada hiyo. Nilijaribu kupinga, lakini nilishambuliwa na kupigwa na kundi la wanaume waliotaka nirushe mchanga kaburini kama ishara ya wema kwa marehemu,” aliongeza.
Mwanamke huyo alikumbuka jinsi alivyopigwa na hata viatu vyake kutupwa ndani ya kaburi.
“Nilikanyagwa, nikapigwa, na hata viatu vyangu vilitupwa na kuzikwa pamoja na mwili wa marehemu,” alisimulia.
Kulingana na mila na desturi za Abagusii, ibada hiyo ya mazishi inamaanisha kuwa mjane anatoa heshima ya mwisho na wema kwa marehemu mume wake.
Baadhi ya imani za kitamaduni pia zinapendekeza kuwa tendo hilo linamfunga mjane kwa mume wake marehemu, na kumzuia kuolewa tena.
“Nilikataa na nikajaribu kukimbilia kwenye shamba la chai lililo karibu, lakini wanaume hao walinifuata na kunikamata kwa nguvu. Walinipiga vibaya. Nilipata majeraha kadhaa wakati wa tukio hilo. Sijui kwa nini waliamua kunifanyia ukatili huo,” alieleza.
Alisema kwamba awali alikuwa amemtuma binamu yake kupeleka watoto kaburini kushuhudia ibada ya mwisho ya baba yao, lakini badala yake, watu wa familia ya mume wake wa zamani walianza kumlazimisha kushiriki katika ibada hiyo.
“Waliniandama na kudai kwamba ni lazima nitie mchanga kaburini kama sehemu ya desturi za mazishi. Walisisitiza kuwa ni lazima nifanye ibada hiyo, ambayo walisema inawakilisha heshima ya mwisho kwa marehemu,” alifichua.
“Nilipokataa, nilishambuliwa, huku wengine wakinishutumu kuwa nilihusika na kifo cha mume wangu wa zamani,” alisema.
Mellen alifichua kuwa kabla ya kifo cha mume wake wa zamani, walikuwa tayari wametengana na hawakuwa wakiishi pamoja.
“Nilihudhuria mazishi ili watoto wangu waweze kumpa baba yao heshima za mwisho. Sikujua kuwa familia ya mume wangu wa zamani walikuwa na nia ya kunidhuru,” alieleza.
Aliongeza kuwa marehemu alikuwa tayari ameoa mke mwingine kabla ya kufariki katika ajali hiyo ya kusikitisha.
Kilichopaswa kuwa tukio la heshima kwa marehemu kiligeuka kuwa fujo baada ya Mellen kushambuliwa huku akipiga mayowe kwa uchungu.
Baba yake Mellen, Nehemiah Mogaka, pia alikumbwa na vurugu wakati wa tukio hilo.
Mogaka aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kiambere.
Hata hivyo, hakuna hatua yoyote ilichukuliwa hadi Jumatatu (Machi 24, 2025) wakati Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, alipoingilia kati.
Mwananchi mmoja alirekodi tukio hilo kwenye video, ambayo ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Video hiyo ilisababisha ghadhabu kubwa na kulaaniwa kote nchini, huku wengi wakielezea kuchukizwa kwao na ukatili huo wa kinyama aliopitia Mellen.
Katika video hiyo isiyo na tarehe, ambayo ilisambazwa kwa kasi mitandaoni, Wakenya walikerwa baada ya kumtazama mwanamke akilazimishwa na wanaume kadhaa kutupa mchanga kaburini kama heshima ya mwisho kwa marehemu mume wake.
Kwenye video hiyo, Mellen anaonekana akipinga, jambo lililomfanya apigwe viboko kaburini.
Baadhi ya watu waliokuwepo eneo la tukio wanasikika wakipiga kelele, wengine wakiomba aachwe huru huku wengine wakishiriki katika kumshambulia zaidi.
Watu waliokuwepo walipiga mayowe huku tukio hilo likiendelea, lakini hakuna aliyejitokeza kumwokoa.
Polisi wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na shambulio hilo.
Jumatatu jioni, Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, alilaani vikali tukio hilo, akifichua kuwa maafisa wa upelelezi wamewakamata baadhi ya wahusika wakuu na wanaendelea kuwatafuta wenzao.
“Nalaani vikali tukio la kikatili lililotokea Nyamira, ambapo mwanamke alifanyiwa unyama na kulazimishwa kushiriki katika ibada ya mazishi ya mume wake wa zamani. Vyombo vya sheria vinachunguza kwa kina ushahidi wote, na wahusika wa kitendo hiki cha kinyama watakabiliwa na mkono wa sheria. Kenya inasimama thabiti dhidi ya ukatili wa kijinsia, na tutahakikisha haki inatendeka kwa mhanga,” alisema Kanja katika taarifa yake.
Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Amin Mohammed, pia alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa watatu waliotambuliwa kama Lameck Osoro, Robert Sarudi, na Bismark Sarudi.
Washukiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya shambulio.